LIPUMBA AIONYA CHADEMA KUHUSU MGOGORO...

Profesa Ibrahim Lipumba.
Chama cha Wananchi (CUF) kimekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumaliza mgogoro wake ili kuweka nguvu kwenye Bunge la Katiba linalotarajiwa kuanza mwakani.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema hayo jana wakati akitoa maoni ya Baraza Kuu la CUF na kuongeza kuwa suala la kupata Katiba mpya yenye misingi imara ya demokrasia na utawala bora linapaswa kupewa kipaumbele na kuunganisha viongozi wa Chadema kulisimamia.
Mgororo ndani ya chama hicho ulitokana na Kamati Kuu (CC) kuwavua nyadhifa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto aliyekuwa  mjumbe wa CC, Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Arusha, Samson Mwigamba, huku wakidaiwa kukabiliwa na mashitaka 11.
"Kwa hali ilivyo sasa na kama itaendelea hivyo, ni dhahiri nguvu kubwa ya Chadema ikaelekezwa kwenye mgogoro wao, jambo ambalo litaathiri ushiriki wao katika mjadala wa Katiba kwenye Bunge la Katiba," alisema Profesa Lipumba.
Alisema katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, Chadema ni miongoni mwa vyama vilivyotoa mchango mkubwa, umoja wao unahitajika kuhakikisha chama hicho kinatumia fursa hiyo muhimu na adimu kwa maslahi ya Taifa.
Aliongeza kuwa wakati mwingine wamekuwa wakifanya kazi na Chadema ili kuhakikisha Katiba mpya inapatikana ikiwa shirikishi na kwamba wakati huu si wa kuendelea kushikana koo wao kwa wao.
Kuhusu kama walishakiandikia chama hicho kutaka kisitishe mgogoro wake, alisema hawajafanya hivyo ingawa yamekuwapo mazungumzo yasiyo rasmi na viongozi hao.
Kuhusu Bunge la Katiba, Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu la CUF linatoa mwito kwa vyama vyenye wabunge kuacha kupigania maslahi yao wakati wa mjadala wa Bunge la Katiba.
"Ni dhahiri, kwamba Katiba inayoandikwa ni ya nchi si chama, hivyo ni muhimu kwa wabunge wa Bunge hilo kuwa wazalendo kwa kutoa michango itakayowezesha kupatikana Katiba bora   badala ya michango itayowezesha kupatikana kwa Katiba yenye maslahi na vyama vyao," alisema Profesa Lipumba.
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la CUF, lilitoa mwito wa kuwapo mkutano wa wadau hususan vyama vya siasa na asasi za kiraia, kujadili Rasimu ya mwisho ya Katiba kwa lengo la kufikia maridhiano kwa mambo muhimu yaliyomo.
Alisema baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha Rasimu ya pili, ni vema wadau wakafanya mkutano utakaorahisishia kazi Bunge la Katiba kufikia mwafaka kuhusu vipengele muhimu vya Katiba mpya.
Hata hivyo, alisema chama hicho kinaamini kuwa Rasimu ya pili ya Katiba Mpya haitakuwa na mabadiliko makubwa kuhusu muundo wa Muungano wa serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya kwanza.
Alisema Baraza Kuu linaamini, kwamba uwepo wa serikali tatu katika muundo wa Muungano ni jambo muhimu na ni njia ya kumaliza kero za Muungano na kuitaka serikali kusimamia kikamilifu mchakato wa Katiba ili ipatikane kabla ya uchaguzi wa 2015.
"Ni wazi, kuwa wananchi hawatakubali kuingia kwenye uchaguzi mwaka 2015 kwa kutumia Katiba ya sasa ambayo imekataliwa na wengi waliotoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba," alisema.
Wakati huo huo, vyama vya wafugaji wa asili  vimemwomba Rais Jakaya Kikwete aangalie kwa makini baadhi ya watu wanaotaka kuharibu  mchakato wa mapendekezo ya wawakilishi kwenye Bunge la Katiba.
Ombi hilo lilitolewa na Mwakilishi wa Mtandao wa Katiba Initiative, Saikon Justin wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mchakato wa kupata wawakilishi tisa ambao wameufanya kwa kushirikiana na mashirika zaidi ya 32 ya vyama vya wafugaji wa asili Tanzania.
Alisema baadhi ya watu wanatumia mchakato wa uundwaji wa Bunge hilo ili wajinufaishe badala ya kuangalia maslahi ya Taifa na wadau wanaopaswa kuchangia kupatikana kwa Katiba mpya.
Aliongeza kuwa  tabia  hiyo inaweza kudhoofisha makundi halisi ya kijamii ambayo yameshiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uandikaji wa Katiba kuanzia hatua  za awali hadi sasa.
Alisema vyama hivyo vilifanya mkutano juzi na kuchagua wawakilishi tisa huku jinsia kizingatiwa kwa wanawake wanne na wanaume watano wenye sifa kuchaguliwa ili kutoa mawazo yao na kuwakilisha wenzao wanaohitaji mawazo yao yawe ndani ya Katiba.

No comments: