MAENEO YA PWANI KUKUBWA NA DHORUBA...

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imehadharisha juu ya kutokea upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa katika maeneo ya pwani mwa bahari ya Hindi leo.
Taarifa iliyotolewa na TMA kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa tukio hilo litatokea leo, wakati wananchi wengi wakisherehekea sikukuu ya Krismasi.
Upepo huo ulielezwa na TMA kwamba ni mkali utakaovuma kilometa 40 kwa saa ambapo  mawimbi ya bahari yanakadiriwa yatazidi kimo cha meta mbili.
Tukio hilo kwa mujibu wa TMA lina uhakika wa kutokea kwa asilimia 60 huku maeneo yatakayoathirika zaidi kuwa ni Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.
"Hali hii inatokana na kuimarika kwa mfumo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika bahari ya Hindi, karibu na visiwa vya Comoro. Mfumo huu unatarajiwa kuvuta upepo kutoka pwani ya Somalia," ilisema taarifa hiyo.
TMA katika taarifa yake iliwahadharisha wakazi wa maeneo hatarishi kuchukua  hadhari ili wasikumbwe na majanga yatakayosababishwa na upepo huo.
Hata hivyo, TMA ilieleza kuwa inaendelea kufuatilia hali hiyo na itatoa taarifa ya mrejeo.

No comments: