Wednesday, October 16, 2013

VYAMA VYA SIASA VYATUMIA SHILINGI BILIONI 167 BILA KUKAGULIWA...

Kabwe Zitto.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi asitishe malipo ya ruzuku kwa vyama vya siasa, hadi uthibitisho wa namna hesabu za vyama hivyo zilivyokaguliwa kwa kipindi cha miaka minne, utakapopatikana.

Vyama vinavyopatiwa ruzuku hiyo ya Serikali, kwa mujibu wa vigezo vya idadi ya wabunge na kura za urais, ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, DP, APPT-Maendeleo na Chausta.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto, alisema kamati yake jana ilishindwa kuendelea na kazi baada ya kupatiwa taarifa na Msajili wa Vyama hivyo pamoja na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuwa hakuna taarifa yoyote ya ukaguzi wa hesabu za vyama hivyo kwa miaka minne sasa.
"Kimsingi hapa kuna kukwepa, sasa tumemuandikia Msajili wa vyama katika kipindi hiki wakati bado hatujapata uthibitisho wa namna hesabu za vyama hivi zilivyokaguliwa kwa miaka minne, ruzuku kwa vyama vyote zisitishwe," alisisitiza Zitto.
Aliongeza kuwa katika muda huo wa miaka minne, Serikali ilitoa Sh bilioni 167 kwa ajili ya ruzuku ya vyama hivyo.
Pamoja na hayo, alimtaka Katibu wa kamati hiyo, aviandikie barua vyama hivyo kufika  mbele ya kamati hiyo na kujieleza ni kwa nini hesabu zao hazijakaguliwa kwa miaka minne tangu 2009, kama Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2009 inavyotaka.
Alisema Sheria hiyo imetamka wazi kuwa ni lazima vyama vyote vya siasa, vinavyopatiwa ruzuku na Serikali, hesabu zake zikaguliwe na ofisi ya CAG, ambapo zamani kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo, vyama hivyo vilikuwa vikitafuta wakaguzi na kujikagua vyenyewe.
"Nimemuita hapa Msajili wa vyama vya siasa atupatie ripoti ya ukaguzi wa vyama hivi vya siasa, lakini ametueleza kuwa hana ripoti hizo, na CAG naye ameeleza hajakabidhiwa bado ripoti hizo, sasa tutaviita vyama hivi vijieleze kwa nini havijakaguliwa hesabu zao lakini wakati huo ruzuku zao zisitishwe kwanza," alisema.
Alidai kwa miaka minne sasa, vyama hivyo vimekuwa vikipokea ruzuku kutoka serikalini, ambapo CCM imepokea Sh bilioni 50.9, Chadema Sh bilioni 9.2, CUF Sh bilioni 6.3, NCCR-Mageuzi Sh milioni 677, TLP Sh milioni 217, UDP Sh milioni 333, DP Sh milioni 3.3, APPT-Maendeleo  Sh milioni 11 na Chausta Sh milioni 2.4.
Alimtaka msajili wa vyama hivyo, kutoa maelekezo kwa vyama hivyo vya siasa kuwa kila chama kinapaswa kutenga fedha katika bajeti yake kwa ajili ya ukaguzi.
"Fedha hizi matumizi yake yanajulikana na yameainishwa baadhi yake ni kutumika katika shughuli za Bunge, jamii na shughuli yoyote muhimu, sasa vyama hivi vinaweza kutumia eneo hili la shughuli yoyote muhimu na kutenga fedha kwa ajili ya ukaguzi," alisema.
Awali, Jaji Mutungi alikiri mbele ya kamati hiyo kuwa hajakabidhiwa ripoti yoyote ya ukaguzi wa vyama hivyo vya siasa; na kusisitiza kwamba kazi ya ukaguzi ni ya CAG ; na si ya ofisi yake.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Benja Majura, alikiri kuwa jukumu la kukagua hesabu za vyama vya siasa, liko chini ya ofisi ya CAG, lakini kutokana na ufinyu wa fedha katika ofisi hiyo, vyama hivyo viliandikiwa barua na kutakiwa kujifanyia ukaguzi vyenyewe na kuwasilisha ripoti kwa CAG.
Alisema baada ya kuandikiwa barua hiyo, vyama viwili vilitafuta wakaguzi ambavyo ni CCM iliyotumia mkaguzi kutoka TAC Association na TLP kilichomtumia mkaguzi kutoka taasisi ya Shebulila, lakini navyo hadi leo havijawasilisha ripoti ya ukaguzi huo.
"Vyama vingine baada ya kuandikiwa kuhusu kujikagua vyenyewe, vilionesha kutoridhika na utaratibu huo kutokana na gharama, lakini ofisi yangu ilishaliona tatizo hili na Februari mwaka huu, tuliandika barua serikalini tukiomba tuongezewe fungu kwa ajili ya ukaguzi huu," alisisitiza.

No comments: