![]() |
Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wawakilishi wa vyama vya siasa Ikulu, Dar es Salaam jana. |
Viongozi waliokutana na Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam katika mazingira ya maelewano na mwafaka, waliongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ndiye msemaji wa viongozi hao.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambao waliungana pamoja kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbali na hao waliotengeneza muungano wao kupinga muswada huo, mkutano huo pia ulihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Mbali na Mangula, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika pia walihudhuria.
Wengine ni Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Mrindoko ambaye anamwakilisha Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema.
Pia, wapo Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa na, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro na Martin Mgongolwa wa NCCR - Mageuzi.
Kabla ya mkutano huo wa jana, NCCR-Magaeuzi, CUF na Chadema, walisitisha maandamano yaliyokuwa yafanyike, kumshinikiza Rais Kikwete asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, uliopitishwa hivi karibuni na Bunge.
Vyama hivyo viliungana kupinga kusainiwa kwa muswada huo, kwa madai kuwa una vipengele vinavyohitaji mabadiliko na ulipitishwa kinyume na taratibu.
Akizungumzia uamuzi huo, Profesa Lipumba alisema umoja huo ulishasikia na kuitambua nia ya Rais Kikwete aliyoionesha katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, ambapo alibainisha wazi kuwa atakutana na viongozi wa vyama hivyo kuzungumzia suala hilo la muswada wa Katiba.
Kutokana na nia hiyo, alisema vyama hivyo havina budi kusitisha kwanza mchakato mzima wa maandamano na mikutano hiyo ya hadhara, hadi mazungumzo na Rais yatakapokamilika na kutoa dira ya kinachoendelea.
Alisema madai ya umoja huo ni kutaka mchakato wa Katiba shirikishi, utakaoheshimu matakwa ya Watanzania wote wa Tanzania Bara na Zanzibar ili kupata Katiba iliyotengenezwa na wananchi wenyewe.
Vyama hivyo kupitia umoja huo, vilipanga kufanya maandamano makubwa kesho, yaliyokuwa yaanzie Tazara na Mwenge hadi Jangwani, kushinikiza kutosainiwa kwa muswada huo wa sheria.
No comments:
Post a Comment