WANAFUNZI 868,030 KUFANYA MiTIHANI YA DARASA LA SABA KESHO...

Baadhi ya wanafunzi wakifanya mitihani wa Darasa la Saba miaka ya nyuma.
Jumla ya wanafunzi 868,030 wanatarajiwa kuanza kufanya mtihani wa darasa la saba kote nchini.

Akitangaza kuanza kwa mtihani huo kesho, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema kati ya watahiniwa wote, wasichana ni wengi ambao ni 455,925 sawa na asilimia 52.52 ya watahiniwa wote na wavulana ni  412,105 sawa na asilimia 47.47.
Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Alisema wanafunzi 844,810 wanatarajiwa kufanya mtihani  huo kwa Kiswahili, kati yao wavulana ni 400,335 na wasichana 444,475.
Wanafunzi 22,535, kati yao wavulana wakiwa 11,430 na wasichana 11,105, wanatarajiwa kufanya mtihani huo kwa Kiingereza ambao ndio walikuwa wakiitumia kujifunzia.
Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 88 wakiwamo wavulana 56 na wasichana 32 ambapo pia watahaniwa 597 wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa wanatarajiwa kufanya mtihani huo.
Mulugo alisema maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, fomu maalumu za OMR za kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo.
Alitoa mwito kwa maofisa elimu wote wa mikoa na halmashauri kuhakikisha utaratibu wote wa mitihani unazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na mazingira kuwa salama na tulivu na kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.
Pia alitoa mwito kwa wasimamizi kufanya kazi yao  kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu kwa kuwa baadhi ya wasimamizi wamekuwa wakishiriki kusaidia watahiniwa kuibia kwenye mitihani yao, na kuonya atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wanafunzi watakaojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mtihani, alisema watawafutiwa matokeo.

No comments: