MELI ZILIZOSAJILIWA ZANZIBAR ZAHATARISHA USALAMA DUNIANI...

Moja ya meli ikisindikizwa kuingia bandarini Zanzibar.
Udhaifu wa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini ya Zanzibar (ZMA) ya mwaka 2006, umeichafua Tanzania katika usafiri wa majini duniani, baada ya sheria hiyo kutoa nafasi ya kusajiliwa ovyo kwa meli za kimataifa bila udhibiti.

Kutokana na udhaifu huo, Tanzania imejikuta ikiwa na meli 400 zinazopeperusha bendera yake duniani, zikiwamo mbovu, zilizouzwa na zilizoondolewa sokoni.
Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini si meli ya mv Gold Star pekee iliyokamatwa na bangi tani 30 yenye thamani ya Sh bilioni 125 hivi karibuni, iliyochangia kuchafua jina Tanzania, bali kumekuwa na meli zingine zilizokamatwa kwa makosa mbalimbali duniani.
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini ya Zanzibar (ZMA) imekuwa ikisajili meli  kupitia wakala wake wa usajili ambaye ni kampuni ya Philtex ya Dubai.
Utaratibu huo,  ulianzishwa baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kujitoa kwenye Sheria ya Usafiri wa Majini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2003, na kuunda sheria yake ya Usafiri wa Bahari ya Zanzibar ya mwaka 2006 ambayo pia iliunda  ZMA.
Sheria ya awali ya Muungano, iliweka masharti ya usajili ambayo ni pamoja na kutoruhusu usajili wa chombo chochote cha baharini chenye umri wa zaidi ya miaka 15.
Aidha, sheria hiyo pia iliweka masharti ya lazima ya kutaka kila chombo cha baharini kinachosajiliwa Tanzania,  kiwe na hisa ya asilimia 50 kwa Mtanzania na lengo likiwa ni kuweka udhibiti wa mchezo mchafu unaoweza kufanywa kupitia vyombo vya kimataifa vya maji.
Hata hivyo, Zanzibar iliikataa na kuunda ya kwake ambayo inaruhusu usajili wa meli yenye umri wowote  bila kipengele cha hisa kwa Mtanzania, hivyo kutoa mwanya kwa meli za nje ya Tanzania kusajiliwa kirahisi.
Kwa Sheria hiyo ya Zanzibar, inayoruhusu meli kusajiliwa na wakala, kampuni ya Philtex, mpaka sasa imesajili zaidi ya meli 400, ikiwamo hiyo ya bangi, zilizowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa (UN) na meli chakavu.
Meli hiyo iliyokamatwa Jumamosi Italia ikiwa na dawa hizo za kulevya, imebainika haikutoka Tanzania, lakini mzigo huo umeichafua nchi kutokana na kuwa na usajili wa Tanzania, kupitia utaratibu wa Zanzibar. 
Akizungumza na mwandishi jana kwa simu, Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Zanzibar, Rashid Seif Suleiman, alikiri meli hiyo kusajiliwa Zanzibar mwaka 2011.
Hata hivyo, alidai katika biashara ya meli, hizo ndizo changamoto ambazo zinaikabili, ya kukosa uwezo wa kutambua mmiliki au wafanyakazi wa meli hizo wanabeba nini.
“Biashara ya meli ni ngumu ukishafanya usajili huwezi kujua wafanyakazi wa meli hizo wanabeba nini, wakati mwingine hata mmiliki wa meli husika hajui, lakini jambo hili tunalifanyia kazi sasa,” alisisitiza Suleiman.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mbali na  mv  Gold Star, kukamatwa Jumamosi iliyopita Italia ikiwa na bangi, nchi hiyo pia Julai 9, ilikamata meli nyingine mv Venus, ikiwa na hali mbaya ya uchakavu kiasi cha kudaiwa kuwa huenda ingezama wakati wowote.
Mv Venus ambayo imesajiliwa kwa utaratibu huo, ilizuiwa kuendelea na safari kutokana na uchakavu.
Tukio lingine lilikuwa la Juni mwaka jana, ambapo meli za Iran, nchi iliyokuwa imewekewa vikwazo vya uchumi na UN, zilitumia udhaifu huo kujisajili kuwa ni za Tanzania ili kukwepa vikwazo vya kimataifa.
Meli hizo za mafuta, zilikutwa zikipeperusha bendera ya Tanzania na kuhatarisha nchi kuingia katika mgogoro, kwa kuwa hatarini kupata adhabu ya UN kwa kuruhusu Iran kupeperusha bendera yake.
Kutokana na udhaifu wa sheria hiyo, Umoja wa Ulaya (EU), kupitia makubaliano ya Paris, Juni ilitangaza Tanzania kuwa moja ya nchi, yenye meli zisizo salama kwa usafirishaji duniani.
Taarifa za uhakika, zimeeleza kuwa kutokana na tangazo hilo la EU, meli yoyote ya Tanzania inayosafirisha mizigo duniani, itakumbana na vikwazo vya kukaguliwa kupita kiasi.
Mwandishi alimtafuta Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ambaye alisema baada ya kupata taarifa za meli hiyo yenye bangi, alizungumza na Waziri wa Zanzibar, Suleiman ambaye alithibitisha kuwa kweli meli hiyo imesajiliwa Zanzibar chini ya Philtex.
“Hata hivyo, amenihakikishia kuwa wako katika mchakato wa kuikatishia mkataba kampuni hiyo wa kusajili meli visiwani humo na suala hilo wanalifanya kwa utaratibu wa kisheria wakiepuka kampuni hiyo kuiburuta Serikali mahakamani,” alisema Dk Mwakyembe.
Mkurugenzi wa ZMA, Abdi Maalim, alibainisha kuwa kupitia Philtex, hadi mwaka jana Zanzibar ilikuwa imesajili meli 400 na kati yao zingine ni mbovu, zimeondolewa sokoni na nzingine kuuzwa na kubaki meli 170 ambazo zinafanya kazi.
Alikanusha mfumo wa usajili na sheria ya Zanzibar vinavyotumika kusajili meli hizo ni dhaifu na kuwa matatizo ya kukamatwa kwa meli hizo yangeweza kutokea mahali popote.
“Hata hivyo, hii sheria tumeifanyia marekebisho na hatusajili tu meli kiholela, kwa zile za abiria zinazosajiliwa ni zenye umri wa chini ya miaka 15 lakini pia tunaangalia ubora na kuzikagua,” alisisitiza.
Alisema ZMA iliingia mkataba na Philtex wa miaka 10 tangu mwaka 2007 ambapo utamalizika rasmi mwaka 2017.

No comments: