MUHIMBILI YAITA WAGONJWA WA MOYO KWA MATIBABU...

Moja ya mitambo ya upasuaji moyo.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ina uwezo wa kufanya tiba zote za upasuaji wa magonjwa ya moyo na hakuna tena haja kwa Serikali kupeleka wagonjwa wote wa maradhi hayo India, imeelezwa.

Kutokana na uwezo huo, uongozi wa hospitali hiyo umeiomba Serikali fedha inazotumia kutibu mgonjwa mmoja nje ya nchi dola 10,000 za Marekani, ili kupeleka wagonjwa hao hospitalini hapo iwatibu kwa dola 6,000.
Akizungumza hospitalini hapo jana na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela, alisema  wametoa ombi hilo kwa maelezo kuwa iwapo Serikali itatumia kituo cha moyo cha Muhimbili, fedha inazotumia kutibu wagonjwa wa moyo nje ya nchi zitaiwezesha   kuimarika zaidi.
Muhimbili imepata uwezo huo baada ya baadhi ya madaktari wake kupata mafunzo   India na Israeli na tangu huduma hizo zianze mwaka 2008 wagonjwa 453 wenye maradhi ya moyo wamefanyiwa upasuaji.
"Upasuaji wa moyo unaofanyika katika hospitali yetu ni sawa na upasuaji  unaofanywa katika vituo vikubwa vya upasuaji moyo duniani kote," alisema jana Dk  Njelekela.
Miongoni mwa huduma zinazotolewa na hospitali hiyo katika kitengo hicho cha moyo ni upasuaji wa kuziba matundu kwenye moyo, kubadilisha valvu ambazo zimebana na kushindwa kuruhusu damu kupita kwenye moyo au kulegea na kufanya damu kuvuja kwenda sehemu isiyohusika na kurudisha moyo katika hali yake ya kawaida ya afya.
Njelekela pia alisema pamoja na kufanya upasuaji, huduma nyingine ambazo zinafanywa na kituo hicho cha moyo ni kliniki za magonjwa ya valvu, moyo kupanuka, mishipa kuziba, mapigo kushuka, magonjwa ya moyo  ya kuzaliwa kwa watoto na upasuaji moyo na mishipa ya damu.
Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa hadi Aprili, Wizara  ya Afya na Ustawi wa Jamii  ilipeleka wagonjwa 402 kupata  matibabu nje ya nchi. Kati yao, 189 walikuwa na matatizo ya moyo, 39 saratani, 34 figo na 140 magonjwa mengine. Wagonjwa hao ni ambao matibabu yao yalishindikana nchini.
Dk Njelekela alisema kituo hicho kina vifaa vya kisasa na vya hali ya juu na mahususi kumudu matibabu ya magonjwa makubwa ya moyo.
"Tunaendelea kutafuta taasisi zenye uzoefu mkubwa wa matibabu ya moyo ili kuanzisha ushirikiano utakaowezesha kupata wataalamu wao kuja kushirikiana na  wa nchini ili kutibu  magonjwa makubwa ya moyo kama njia ya kuongeza uwezo kitaaluma.
Alisema Serikali imetoa fedha kununulia mtambo mkubwa wa kuchunguza mishipa na shinikizo ndani ya moyo na maradhi makubwa ya moyo ya kuzaliwa.
"Huu ndio mtambo ambao kwa kipindi kirefu umekuwa ukisababisha Serikali kupeleka wagonjwa wengi wa moyo India," alisema Dk Njelekela na kuongeza kuwa mtambo huo ambao umenunuliwa kwa Sh bilioni 3.6 ulifungwa hivi karibuni na wataufanyia majaribio mwezi ujao.
Alisema ndio unaosaidia kuangalia mishipa ya damu inayokwenda kwenye moyo na kuangalia moyo unavyofanya kazi na pia kama mtu anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali hiyo, Agnes Kuhenga alisema  mgonjwa mwenye rufaa kutoka hospitali za mikoa atatibiwa kwa Sh 10,000 kumwona daktari, Sh 20,000 akilazwa na akifanyiwa upasuaji atalipa Sh 50,000.
Pia alisema kutokana na sera ya msamaha, wagonjwa watachujwa kuhakikisha hakuna matumizi mabaya ya sera hiyo. Alisema wataweka utaratibu wa kuomba Serikali kutoa fedha zote kwa hospitali kwa wagonjwa watakaopewa huduma kwa njia ya msamaha.
Pia Kuhenga alisema kuna wagonjwa wa kulipia (private) ambao ni wateja  wenye uwezo wa kulipia fedha taslimu au kupitia bima za afya ambazo zipo sasa.
Mkuu wa Kituo hicho, Dk Robert Mvungi alisema kina uwezo wa kulaza wagonjwa 88 kwa wakati mmoja vikiwamo vitanda vyenye hadhi ya kulaza viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Rais.
"Juzi alikuja kutibiwa hapa Rais wa Comoro ... tuna vitanda vyenye hadhi hiyo," alisema Mvungi na baadaye waandishi wa habari walijionea vyumba vya upasuaji vilivyo na hadhi na mitambo ya hali ya juu.

No comments: