WALIOJERUHIWA SHAMBULIO LA KENYA SASA WAFIKIA 162, AL-SHABAAB YAKIRI KUHUSIKA...

Askari wa Jeshi la Kenya wakiwa wamejipanga nje ya jengo hilo.
Mmoja wa majeruhi akipatiwa msaada na wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu.
Habari zilizopatikana muda mfupi uliopita zinasema idadi ya majeruhi katika shambulio la uvamizi wa jengo la maduka la Westgate nchini Kenya imefikia zaidi ya 162 huku kundi la al-Shabaab lilitangaza kuhusika na tukio hilo.
Wakati idadi ya majeruhi ikifikia hapo, watu waliokufa mpaka sasa inaaminika kufikia zaidi ya 40.
Polisi na wanajeshi nchini humo wameweza kudhibiti ghorofa ya kwanza na ya pili kwenye jengo hilo, huku wito ukitolewa na mamlaka husika kwa watu kujitokeza kwenda kuchangia damu kwa ajili ya majeruhi wa tukio hilo.
Inaaminika bado kuna mamia ya watu wa mataifa mbalimbali waoshikiliwa mateka ndani ya jengo hilo wakati milio ya risasi imeendelea kusikika ndani ya jengo hilo.
Rais Uhuru Kenyatta amewataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki na kuahidi askari wake watawashinda wavamizi hao ndani ya kipindi kifupi kijacho.
Tayari serikali ya Canada imethibitisha vifo vya raia wake wawili akiwamo mfanyakazi wa Ubalozi wake nchini Kenya.

No comments: