SHAMBULIO LILILOUA WATU 39 KENYA LILIWALENGA WASIOKUWA WAISLAMU...

KUSHOTO: Askari wa Kenya akijiandaa kukabiliana na wavamizi hao jana. JUU NA CHINI: Baadhi ya majeruhi wakisaidiwa kutoka kwenye jengo hilo.
Takribani watu 39 wameripotiwa kufa na zaidi ya 50 kujeruhiwa wakati polisi walipotupishiana risasi na watu wenye silaha katika eneo moja la maduka kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Mmoja wa mashuhuda alidai watu hao wenye silaha waliwataka Waislamu kusimama na kuondoka eneo hilo na kwamba walengwa pekee ni wale wasio Waislamu wakati walipomimina risasi kwenye jengo hilo la ghorofa lenye maduka lililopo kwenye wilaya ya Westlands majira ya mchana jana.
Zaidi ya watu 30 waliojeruhiwa na kufa, walibebwa nje na walinzi kwa kutumia vitanda maalumu vya wagonjwa na kwenye matoroli ya kubebea bidhaa, wakati wengine walionekana wakitoka nje ya jengo hilo, wakiwa wametapakaa damu kwenye nguo zao kuzunguka majeraha yao.
Raia na watalii ambao walikuwa wakifanya manunuzi ya Jumamosi nchini Kenya walikimbia huku wakipiga mayowe kutoka kwenye jengo hilo na magari yalitelekezwa huku washambuliaji hao wakitupa mabomu na kumimina risasi kutoka kwenye bunduki zao aina ya AK47.
Kwa zaidi ya saa moja watu waliongozana kutoka kwenye jengo hilo, huku zaidi ya 10 wakiwa wametapakaa damu na kuwakumbatia watoto wadogo.
Taasisi ya Msalaba Mwekundu nchini Kenya imesema kwamba 39 wameripotiwa kufa na takribani 50 wamejeruhiwa.
Takribani watu tisa walichukuliwa nje ya jengo hilo wakichuruzika damu kutoka kwenye majeraha yao miguuni na wengine wawili walibebwa wakiwa hawajitambui kutoka eneo ya tukio ndani ya matoroli ya kubebea bidhaa.
Mvulana mdogo anaaminika kuwa ni miongoni mwa waliouawa.
Katibu Mkuu wa Msalaba Mwekundu Kenya, Abbas Guled alisema: "Majeruhi ni wengi, na hawa ndio pekee tulionao nje. Kule ndani kuna wengi zaidi na majibizano ya risasi bado yanaendelea."
Hakukuwa na uthibitisho wa ripoti za milipuko miwili mikubwa, sambamba na milipuko kadhaa midogo. Watu wawili waliripotiwa kujeruhiwa barabarani.
"Tuna maofisa katika eneo la tukio wakijaribu kukabiliana na kundi linafyatua risasi ndani. Hawajajulikana walikojibanza," alisema polisi mmoja wa ngazi ya juu.
"Polisi wanakabili hali hii kwa tahadhari sababu kuna wananchi wasio na hatia ndani," alisema.
Polisi wenye silaha waliwasili katika eneo la tukio karibu nusu saa baadaye na waliweza kusikia sauti 'toka nje, toka nje' huku idadi kubwa ya wateja ikilikimbia jengo hilo.
Mfanyakaziwa Ubalozi wa Uholanzi Rob Vandijk alisema alikuwa akila kwenye mgahawa mmoja ndani ya jengo hilo ndipo watu wenye bunduki walipotupa bomu la mkono ndani ya jengo hilo.
Watu walianza kupiga mayowe na kulala chini, alisema, huku bunduki zikirindima kila kona ya jengo hilo la maduka lenye pilika nyingi.
Maofisa hawajatoa idadi halisi ya vifo huku polisi na wavamizi hao wakiendelea kutupishiana risasi, lakini waandishi walisema walishuhudia takribani miili 15.
Polisi wamesema kwamba washambulizi hao wanawashikilia mateka saba ndani ya jengo hilo, na watu wengine wamebaki mafichoni ndani.
"Niliwaona washambulizi watatu wakiwa wamevalia mavazi meusi na kujifunika sura zao na walikuwa wamebeba silaha nzito," alisema shuhuda mwingine.
Wanajeshi wa Kenya pia walipelekwa kushiriki katika operesheni ya kulirejesha jengo hilo chini ya udhibiti.
Helikopta za polisi zilizunguka juu ya jengo hilo huku mirindimo ya risasi ikiweza kusikika zaidi ya masaa mawili baada ya shambulio hilo kuanza.
Polisi walifunga barabara zinazozunguka jengo hilo zilizoko karibu na eneo la katikati ya Nairobi la Westlands.
Manish Turohit, miaka 18, ambaye alitoroka baada ya kujificha katika karakana ya maegesho kwa masaa mawili, anasema aliona watu wenye silaha wakiwa na bunduki za aina ya AK47 na wamejizingira na mabomu ya mkono ndani ya jengo hilo.
Polisi mwanzoni waliamini shambulio hilo lilikuwa jaribio lililopangwa na watu kumi wenye silaha kupora duka moja.
Lakini Elijah Kamau, shuhuda, alieleza kwamba watu hao wenye silaha walitangaza kwamba walikuwa wamewalenga wasiokuwa Waislamu wakati wakianza shambulizi lao kwenye jengo hilo.
Baadhi ya wote walionusurika 'walipewa sharti la kukariri sala za Kiislamu na kisha kuruhusiwa kutoka nje', kwa mujibu wa Allan Sayers na kusema alikuwa kwenye jengo la Westgate dakika tano baada ya shambulio hilo.
Sayers alisema watu walikuwa bado wakiwasiliana na baadhi ya mateka kwa simu na meseji.
"Bado kuna mateka wengi ndani na ripoti za wengi zaidi waliokufa," alisema.
Mkuu wa Polisi wa Nairobi, Benson Kibue amesema lilikuwa shambulio la kigaidi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imesema kutupishiana risasi huko kunaweza kuwa 'shambulio lililofanywa na magaidi'.
"Hawaonekani kama wahuni, hili zi tukio la ujambazi," alisema Yukesh Mannasseh ambaye alikuwa kwenye ghorofa ya juu wakati kutupishiana risasi huko kulipoanza.
"Inaonekana kama shambulizi. Walinzi waliowaona walisema walikuwa wakifyatua risasi kama wamepagawa."
Kundi la maharamia wa Kisomali la al-Shabaab liliapa mwishoni mwa mwaka 2011 kufanya shambulizi kubwa zaidi mjini Nairobi katika kulipiza kisasi cha kitendo cha Kenya kupeleka vikosi vyake nchini Somalia kupambana na askari waasi wa Kiislamu.
Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabaab mapema lilitishia kushambulia jengo hilo, kutokana na kuwa kitovu maarufu kwa jamii ya kigeni jijini humo.
Hata hivyo, mpaka sasa hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo .
Mwathirika mmoja alisema alipigwa risasi na mtu mmoja ambaye alionekana kuwa Msomali, wakati wengine walibainisha watu hao wenye silaha walikuwa wakizungumza lugha ya kigeni.
"Watu hao wenye silaha walijaribu kunipiga risasi kichwani lakini wakanikosa. Hakika kuna majeruhi wengi mno," alisema Sudjar Singh, ambaye anafanya kazi katika jengo hilo la maduka.

No comments: