TANZANIA NA RWANDA SASA ZAAFIKIANA USHURU WA BARABARA...

Baadhi ya malori yaendayo nchini Rwanda yakiwa safarini.
Hatimaye Rwanda na Tanzania zimefikia mwafaka kuhusu  ushuru wa barabara, ambapo nchi hizo zimeshusha viwango vya kodi na sasa kutoza dola 152 za Marekani, bila kujali umbali.

Akizungumza na mwandishi kwa simu akiwa Kampala, Uganda jana, baada ya kumaliza mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango wa Rwanda, Claver Gatete, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, alisema mwafaka umefikiwa.
“Tumefikia mwafaka kuhusu suala hili, na wenzetu wamekubali kushusha kodi yao mpya waliyokuwa wakitutoza Tanzania pekee kutoka dola 500 hadi 152 na sisi pia tumeshusha kutoka dola   216 hadi 152,” alisema Mgimwa.
Awali Tanzania ilikuwa inatoza dola 16 kwa kilometa 100 kwa magari yanayosafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam, kwenda nchi zisizo na bahari.
Alisema Tanzania imebidi iridhie kushusha kiwango hicho kutokana na ukweli kuwa endapo Rwanda ingeendelea kutoza kiwango hicho kipya, wafanyabiashara wa Tanzania ndio wangeathirika zaidi kutokana na wingi wa magari ya mizigo yanayokwenda Kigali, kuliko yanayotoka Kigali kwenda Dar es Salaam.
“Kwa hesabu za haraka malori ya mizigo yanayotoka Tanzania kwenda Kigali kwa siku, yanafikia 200 hadi 300, wakati yanayotoka Kigali kwenda Tanzania ni 20 hadi 30,” alisisitiza.
Awali Tanzania ilikuwa ikitoza ushuru wa dola 16  kwa lori kwa kilometa 100 na Rwanda ikaamua kutoza ushuru huo huo. Hata hivyo, baada ya muda Rwanda ilibaini kuwa haipati faida kama Tanzania.
Tanzania kwa ushuru huo, kutoka Dar es Salaam hadi Rusumo mpakani mwa Tanzania na Rwanda, umbali wa kilometa 1,389, ilikuwa ikipata dola 216, wakati Rwanda kwa ushuru huo, kutoka Rusumo hadi Kigali umbali wa kilometa 139, ilijikuta ikiambulia dola 22.24 tu kwa gari.
Kutokana na mazingira yaliyoonekana ya kukosa uwiano sawa  na Tanzania, yaliyotokana na udogo wa nchi husika, Rwanda ilipandisha ushuru na kuwa dola 152 bila kujali umbali, kwa kuwa kijiografia haukuwa na msaada kwao.
Hata hivyo, Tanzania haikulalamika kwa ongezeko hilo la ushuru na iliendelea kufanya biashara na Rwanda kama inavyofanya na nchi zingine zinazopitisha mizigo yao Dar es Salaam.
Juzi alipozungumza na mwandishi kuhusu kikao hicho cha kujadili mustakabali wa kodi hiyo ya barabara Waziri Gatete, alikiri kuwa Serikali yake iko tayari kupunguza kodi endapo kutakuwa na ushuru linganifu.
Alisema nchi yake kwa takribani miaka mitatu sasa imekuwa ikilalamikia utofauti wa kodi za barabara baina yake na Tanzania ambapo kodi inayotozwa Tanzania ni kubwa kuliko ya Rwanda, jambo lilisababisha wapandishe kiwango hicho ili kupata ulinganifu.

No comments: