MSIKITI WA MANYEMA WAUNGUA MOTO DODOMA...

Msikiti wa Manyema  uliopo mtaa wa saba mjini hapa jana ulishika moto na kusababisha mtafaruku miongoni mwa waumini ambao walikuwa wanaondoka eneo la msikiti baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa.

Mashuhuda wamesema moto huo ambao ulidhibitiwa na Kikosi cha Zimamoto ulianzia katika maungio ya waya wa umeme.
Watu hao walisema kwamba moto huo ulionekana kutokea katika swichi na kusambaa katika ghorofa ya juu.
Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dodoma, Damas Nyanda aliyefika na kujionea hali halisi alisema hawajapata taarifa ya majeruhi au hasara iliyopatikana kutokana na moto huo.
Alisema wanasubiri tathmini ya uongozi wa msikiti huo juu ya hasara iliyopatikana.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto Mkoa, Sajini Amiry Issa alisema walifika dakika 4 baada ya kupokea taarifa ya ajali hiyo ya moto na kukuta moto umesambaa maeneo mbalimbali ya msikiti huo wenye ghorofa moja.
Issa alisema urahisi wa kuzima moto huo ulitokana na wao kupewa taarifa mapema kabla ya moto kusambaa na kuleta madhara makubwa.
Mwandishi alishuhudia Mazuria yanayotumiwa kuswali, vitabu, kanzu na nafaka iliyokuwa ghorofa ya juu ikiwa imeunguzwa na moto huo uliozuka kuanzia majira ya saa 8. 10 mchana.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema baada ya swala ya Ijumaa watu waliokuwa nyuma walishtukia moshi mkubwa ukisambaa kutokea juu ya msikiti huo.
Mmoja wa waumini hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Said alisema waliona moto huo ukianzia juu kwenye maungio ya umeme.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa  wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi ameagiza uongozi wa mkoa kukutanisha wataalamu wa uhandisi, ujenzi, Zimamoto, Tanesco na wataalamu wa afya ya wanadamu ili kutathmini jengo hilo la msikiti lililoungua kama lina usalama kuendelea kutumika.
Taarifa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa imesema kwamba taarifa hiyo inatakiwa ikamilike kufikia leo.
Aidha uongozi wa mkoa umeamua kutoa msaada wa vyakula kwa ajili ya kusaidia hapo msikitini. Msaada huo una thamani ya Sh 300,000.
Msikiti huo una watoto kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao wanaelezwa kuchukua mafunzo ya dini.

No comments: