JWTZ YASEMA: TANZANIA HAIPIGANI NA WAASI, INALINDA AMANI DRC...

Askari wa waasi wa M23 wakiwa kwenye doria.
Jeshi  la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema Tanzania haipigani na waasi wa M23 na haina tatizo na Rwanda kuhusu Operesheni ya Ulinzi wa Amani inayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ridhaa ya kikosi hicho kwenda DRC ilitolewa pia na Rwanda, nchi ambayo ni mwanachama wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ambayo imesaidia sana kwa kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha watu, vifaa na zana kwenda DRC.
Msemaji wa Jeshi hilo, Meja Erick Komba alisema hayo jana kutokana na habari za kupotosha zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kikosi cha jeshi hilo kupigana na M23.
Alitaka ieleweke kuwa kikosi cha Tanzania kilicho DRC ni sehemu ya Brigedi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyotoa mchango katika Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO).
"Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu kiko chini ya majeshi ya MONUSCO, inamaanisha kuwa operesheni hiyo ni ya Umoja wa Mataifa,” alisema.
Alisisitiza kuwa kikosi hicho kinafanya kazi chini ya MONUSCO kikiwa na majukumu ya kuzuia waasi, kuvunja nguvu za waasi na kupokonya silaha makundi yote ya waasi.
"Kwa mantiki hiyo ieleweke kuwa ushiriki wa Tanzania katika operesheni unatokana na mgogoro kati ya Serikali ya DRC na waasi, hususan kikundi cha waasi cha M23," alisema Komba.
Alisema mgogoro huo ulianza Aprili mwaka jana baada ya kikundi cha M23 kujitoa kwenye Jeshi la DRC na kuanzisha mapigano, hali iliyofanya usalama DRC kuwa mbaya.
Komba alisema kutokana na hali hiyo ya usalama, wakati wa kikao cha viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu cha Julai 12, mwaka jana Addis Ababa, Ethiopia, Rais Joseph Kabila aliwasilisha ombi kwa wakuu wa nchi za Rwanda, Uganda na Tanzania zisaidie kuwapokonya silaha waasi wa M23.
Alisema wakuu wa nchi hizo walikubaliana na ombi hilo na kutoa maelekezo kwa mawaziri wa ulinzi kuyajadili.
Alisema mawaziri walikubaliana kuwa ni muhimu kwa vikundi vyote vya waasi (ADF, FDLR na M23) kushughulikiwa na waliwasilisha mapendekezo yao kwa wakuu hao.
Alisema baadaye taarifa hiyo iliwasilishwa kwa wakuu hao ambao waliagiza kushirikishwa kwa nchi wanachama wa SADC, Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) ili kufanikisha mkakati huo.
Komba alisema nchi za SADC na za Maziwa Makuu kwa pamoja zilikubaliana na kupendekeza Brigedi ya SADC ipelekwe DRC kama Kikosi Maalumu cha Kulinda Usalama (NIF).
"Kutokana na ridhaa hiyo nchi wanachama wa SADC ziliombwa kuchangia na kukubali, lakini UN ilipitisha nchi za Tanzania, Afrika Kusini na Malawi kuchangia askari na kuunda NIF ya MONUSCO.
Aidha, UN mwaka huu iliridhia mapendekezo ya wakuu wa nchi za Maziwa Makuu na wanachama wa SADC kuundwa NIF na kupelekwa DRC.
Kwa idhini hiyo, Machi 28 Baraza la Usalama la UN lilipitisha Azimio namba 2098 (2013) na kutoa jukumu maalumu la ulinzi wa amani DRC, likijumuisha ushiriki wa NIF kama sehemu ya MONUSCO na kuitwa Brigedi ya Majeshi ya Kulinda Amani ya UN (FBI) yenye mamlaka ya kujibu mapigo ambayo kikosi cha Tanzania ni sehemu ya Brigedi hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, Assah Mwambene alisema hakuna ugomvi wowote kati ya Tanzania na Rwanda na kuasa baadhi ya vyombo vya habari hasa magazeti, kuacha kuandika habari za uchochezi.
Alitaka magazeti yasiwe sehemu ya kuchochea uwepo wa majeshi ya Tanzania Mashariki mwa DRC kama ni majeshi yanayojitegemea bali yako chini ya  UN.
"Kwa kuandika habari hizo, inaleta taswira mbaya na kuchanganya wananchi kwa kuandika hasa vichwa vya habari vya uchochezi," alisema.

No comments: