NI KWELI SHEKHE PONDA AJERUHIWA BEGANI, ANATIBIWA MUHIMBILI...

Shekhe Ponda Issa Ponda akiwa wodini katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katibu wa Jumuiya ya Taasisi ya Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, baada ya kujeruhiwa bega la kulia. Jeraha hilo inadaiwa amelipata katika jaribio la Polisi kutaka kumkamata mkoani Morogoro.

Taarifa ya Msemaji wa Polisi, Advera Senso, iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa Shekhe Ponda yuko katika hospitali hiyo, akitibiwa jeraha katika bega la mkono wa kulia.
Kujeruhiwa kwa Shekhe Ponda kwa mujibu wa Senso, kumesababisha Polisi kuunda timu yenye wajumbe kutoka Jukwaa la Haki Jinai, wakiongozwa na Kamishna wa Polisi, CP Issaya Mngulu, kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
Aidha, Polisi imetoa mwito kwa wananchi kuwa watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa kisheria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Polisi, juzi wakati wa Sherehe za Iddi Pili, baada ya kufungwa kwa Kongamano la Kidini lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu mkoani Morogoro, askari Polisi walijaribu kumkamata Shekhe Ponda bila mafanikio ambapo alitoroshwa na wafuasi wake.
“Baaada ya askari kutaka kumkamata, wafuasi wake walizuia ukamataji huo kwa kuwarushia mawe askari, hata hivyo askari walipiga risasi hewani kama onyo la kuwatawanya lakini wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha mtuhumiwa,” taarifa hiyo ilieleza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jaribio la kumkamata Shekhe Ponda, lilifanyika kwa tahadhari baada ya watu waliohudhuria kongamano hilo kutawanyika, huku baadhi ya wafuasi wa Shekhe huyo, wakiwa wamezingira gari dogo alilokuwa amepanda.
“Askari Polisi walizuia gari hilo kwa mbele kwa nia ya kutaka kumkamata Shekhe Ponda,” ilieleza taarifa hiyo na kuongeza kuwa lengo la kumkamata, ilikuwa tuhuma dhidi yake za uchochezi.
“Mpaka sasa anatuhumiwa kwa kosa la kutoa maneno ya uchochezi sehemu mbalimbali hapa nchini, yenye lengo la kusababisha uvunjivu wa amani,” ilieleza taarifa hiyo.
Awali kabla ya taarifa hiyo ya Senso, Polisi mkoani Morogoro, ilikanusha uvumi uliosambazwa katika mitandano ya jamii kuwa Shekhe Ponda, amefariki dunia  kwa  kupingwa risasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilongile, akizungumzia vurugu hizo jana, alisema Shekhe Ponda alialikwa pamoja na mashehe wengine wanne kutoka jijini Dar es Salaam katika kongamano hilo.
Alidai Shekhe Ponda alikuwa mtu wa mwisho kupanda jukwaani, zikiwa zimesalia dakika 10 kabla ya kumalizika muda wa baraza hilo na alitumia dakika tano kuzungumza na waumini hao.
Kamanda Shilongile alisema wakati wote askari Polisi walikuwepo katika eneo la kongamano hilo ambalo lilikuwa halali, baada ya kupatiwa kibali.
Hata hivyo kwa mujibu wa madai ya Kamanda Shilongile, kibali hicho kilikuwa na masharti ya kutoruhisiwa kwa Shekhe Ponda, kwa kuwa  alikuwa akitafutwa kwa tuhuma mbali mbali zikiwemo za uchochezi na uvujivu wa amani Dar es Salaam na Zanzibar.
“Lengo la Polisi ni kukumkatama kutokana na makosa aliyoyatenda Dar es Salaam na Zanzibar ... hatukutaka kutumia nguvu ili kuepusha maafa ya watu zaidi ya 3,000, lakini tulishindwa kumkamata, alitoroshwa na waumini wake,“ alidai.
Kutokana na baadhi ya waumini hao kuwazuia askari kufanya kazi yao ya kumkamata Shekhe Ponda, Polisi inawashikilia watu wawili kwa kosa hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadalizi ya kongamano hilo, Ustaadhi Idd Msema, alidai Shekhe Ponda baada ya kongamano hilo alipanda katika gari dogo kwenda katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja, alipoteremka ili kuingia msikitini, alifyatuliwa risasi iliyopiga kwenye bega la kulia.
Alidai kuwa baada ya kupigwa risasi begani, waumini walimchukua na kumpakiza katika piki piki hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro  kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Baada ya kufika hapo kwa mujibu wa madai hayo, waliona hakuna daktari  wa kumpatia matibabu, ndipo walipoamua kumwondoa na kumpekea katika zahanati ya taasisi ya dini, ambayo hakupenda kuitaja, ili apate huduma ya kwanza.
“Hatuwezi kutaja anapotibiwa Shekhe Ponda kwa ajili ya usalama, hasa wakati huu ambapo kumekuwa na sintofahamu,“ alisema Mwenyekiti huyo.
Baadhi ya walinzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro waliozungumza na gazeti hili, walikiri kuwa Shekhe Ponda alipelekwa hapo kwa usafiri wa piki piki joini ya siku hiyo, akisindikizwa na baadhi ya waumini waliokuwa na pikipiki zaidi ya 50.
Kwa masharti ya kutotaja majina yao, walinzi hao walidai kuwa waumini hao walimbeba Shekhe Ponda na kuingia naye kwa nguvu hadi mapokezi, na walinzi hao walitoa taarifa Polisi kuhusu umati huo na baadhi ya waumini walioanza kurusha mawe.
Walidai muda si mrefu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),  waliwasili na gari lao hospitalini hapo na kuwatawanya watu hao.
Hata hivyo walinzi hao walidai, watu waliokuwa akishughulikia matibabu ya Ponda mapokezi baada ya kuona askari wamefika hospitalini hapo, walimyanyua Shekhe Ponda na kutokea mlango mwingine unaotazamana na Kanisa Kuu Katoliki, Jimbo la Morogoro, na kuondoka naye kwa usafiri wa pikipiki kwenda kusikojulikana.

No comments: