WAKIMBIZI HARAMU ZAIDI YA 7,000 WAREJESHWA KWAO...

Baadhi ya wakimbizi wakiwa njiani kurejea makwao.
Baada ya agizo la Rais Jakaya Kikwete kutaka wahamiaji haramu kuondoka kupata mafanikio, muda wowote kuanzia sasa operesheni maalumu kusaka waliokaidi itaanza.

"Vyombo vya Dola muda wowote vitaanza operesheni katika maeneo ambayo yalihusika na agizo hilo ambalo makataa yake ya siku 14 yalimalizika jana," chanzo chetu cha habari ambacho hakikutaka kutajwa kilisema.
Akiwa katika sherehe za Siku ya Mashujaa Julai 25 katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kaboya wilayani Muleba, Rais alitoa agizo la wahamiaji hao kuondoka na mifugo yao.
Alitaka pia wanaoendesha ujambazi na ufugaji haramu katikati ya msitu hasa katika mikoa ya Kagera, Geita na kwingineko nchini kuondoka mara moja na mifugo yao na pia wasalimishe silaha walizonazo ambazo zimekuwa zikitumika kwa uhalifu.
Chanzo kilisema hadi jana wakimbizi haramu 6,780 walishaondoka kurudi kwao, kati yao 4,377 wakiwa ni Wanyarwanda, 2,219 Warundi na 174 Waganda.
Kilisema pia kuwa pamoja na wakimbizi hao kurudi kwao, bunduki 21 zilisalimishwa ikiwamo moja aina ya SMG, ambapo pia mifugo wapatao 5,000 wakiwamo ng'ombe, mbuzi na kondoo, walithibitika kuvuka mipaka kurudi walikotoka wakimbizi hao.
"Mifugo waliokuwa msituni wanakadiriwa kuwa 53,000, lakini wapo waliorudi kupitia njia za panya," kilisema chanzo hicho ambapo pia mwandishi wa habari hizi aliyekuwa maeneo ya mpakani alishuhudia maofisa wa Serikali ya Rwanda wakifuatilia kwa makini urejeaji wa wananchi wao.
Kuhusu idadi ya waliorejea kupitia njia zisizo rasmi, chanzo chetu kilisema inasemekana ni zaidi ya 20,000 ambao hawakutaka kupitia katika vituo halali ambavyo ni maalumu kwa kupokea wakimbizi hao.
Licha ya nchi zenye wakimbizi hao haramu nchini kulalamika kuwa pengine kulikuwa na lengo hasi kurudisha wakimbizi hao, Serikali ya Tanzania iliendelea kusisitiza kuwa lengo ni la kiusalama na si kumlenga mtu au nchi yoyote.
Uamuzi wa Rais Kikwete kutoa agizo hilo, ulitokana na kuibuka na kukithiri kwa wimbi la ujambazi na utekaji nyara wa abiria waliokuwa wakisafiri kwa mabasi kupitia baadhi ya barabara za mipakani.
Jambo hilo lilimshangaza Rais Kikwete hasa alipoambiwa kuwa abiria wamekuwa wakilazimika kusindikizwa na polisi wanapopitia njia zilizo karibu na misitu hususan katika wilaya ya Biharamulo kuchelea kutekwa nyara na majambazi ambao wengi wao walishabainika kuwa raia wa kigeni.
Akizungumza jana na mwandishi kuhusu hatua hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi alithibitisha baadhi ya wahamiaji hao   kuondoka.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa pori ni kubwa, asingeweza kupata idadi kamili ya walioondoka lakini akasisitiza pia kuwa operesheni maalumu itaanza ili 'kufagia' waliosalia porini humo.

No comments: