KUSHOTO: Shekhe Ponda Issa Ponda akiwa hospitalini. KULIA: Wafuasi wa Shekhe Ponda wakilizingira gari la polisi mkoani Morogoro. |
Wakati Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Dar es Salaam, likilaani kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI), imeshindwa kubaini kilichomjeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Moi, Jumaa Almasi, alisema uchunguzi wa wataalamu wa taasisi hiyo, alikolazwa Shehe Ponda ambako alifanyiwa upasuaji upya, umeshindwa kubaini kilichomjeruhi.
"Kutokana na tiba ya awali aliyopewa, ikiwa ni pamoja na kushonwa jeraha kabla ya kufikishwa Moi, imekuwa vigumu kujua jeraha lilisababishwa na kitu gani," alisema Almasi.
Mbali na kutojua kilichomjeruhi Ponda, Almasi alisema hali ya Shehe Ponda anaendelea vizuri, ikilinganishwa na alivyokuwa kabla ya kufikishwa hospitalini hapo juzi.
Kwa mujibu wa Almasi, Ponda alifikishwa katika kitengo hicho juzi saa 7.30 mchana akitoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Alisema baada ya kupokewa, Shehe Ponda alionekana na jeraha mgongoni chini ya bega la kulia, lililokuwa limeshonwa mbele na nyuma na baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi walishauri afanyiwe kipimo cha x-ray ili kubaini kama kuna mvunjiko kwenye sehemu ya jeraha.
"Tathimini ya madaktari baada ya kupata majibu ya x-ray, ilionesha alikuwa na mvunjiko bila mifupa kupishana, vivyo hivyo kidonda hakikuwa katika hali nzuri. Hivyo licha ya tiba aliyopewa mwanzo, iliamuliwa afanyiwe upasuaji mpya ili kuzuia maambukizi kama kingeachwa hivyo," alisema Almasi.
Kuhusu ulinzi wa Polisi kwa kiongozi huyo, Almasi alisema haoni kama kuna ulinzi uliowekwa kwa kiongozi huyo kwa kuwa hata chumba alimolala kwa matibabu yuko peke yake.
"Askari wanakuja na kuondoka, sasa sijui kama kuna mtu anamlinda, chumba alimo yuko huru É zaidi ya hapo sidhani kama naweza kusema jambo lingine zaidi kuhusu ulinzi huo," alisema Almasi.
Mwandishi alishuhudia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, akiingia ndani ya taasisi hiyo na kuondoka, lakini haikufahamika kama alikwenda kumwona Shehe Ponda au alikuwa na shughuli zingine.
Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam, ililaani tukio la kujeruhiwa kwa Shehe huyo.
Bakwata ilimtaka Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, akae pembeni wakati timu yenye wajumbe kutoka Jukwaa la Haki Jinai, wakiongozwa na Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu, ikifanya kazi yake ya uchunguzi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, alisema wamesikitishwa na tukio hilo kutokana na mazingira yake yaliyohusisha Polisi.
Shehe Salum alitaka timu iliyoundwa kufanya uchunguzi, kuwa huru na itende haki, huku akibainisha kuwa ikithibitika kuwa polisi walimpiga risasi Shehe Ponda, italeta chuki kati ya Waislamu na Polisi.
Kwa mujibu wa Shehe Salum, hakukuwa na haja ya kiongozi huyo kupigwa risasi hata kama alikuwa na kosa.
"Ponda si jambazi, tunaamini Jeshi la Polisi lina weledi mkubwa katika kazi yake, lingemkamata katika mazingira mengine yoyote tangu akiwa Zanzibar hadi Morogoro na si kwa risasi, tunaomba haki itendeke katika hili na polisi aliyehusika achukuliwe hatua," alisisitiza Shehe Salum.
Alisema tofauti zilizopo kati ya Bakwata na Shehe Ponda si uadui, bali mitazamo ya kifikra ambayo haipaswi kutafsiriwa vibaya katika jamii kuwa pengine pande hizo zina uhasama.
Shehe Salum alisema ili kulinda heshima na amani kwa Taifa, ni vema timu ifanye kazi yake kwa weledi mkubwa, na kutoa majibu sahihi juu ya nani alihusika kumjeruhi Ponda, ili hatimaye sheria ichukue mkondo wake.
"Tunaomba wakati uchunguzi wa tukio hili ukiendelea, Shilogile ajiuzulu ili haki itendeke na ikithibitika kuwa Polisi wamehusika, basi askari aliyempiga risasi na aliyemwamuru, washitakiwe," aliongeza Shehe Salum.
Alisema kitendo cha kiongozi huyo kujeruhiwa wakati akiwa katika mkutano huku polisi wakitajwa kuhusika, hakileti picha nzuri na hata kama alikuwa akitafutwa, polisi walijua mahali gani wangempata, hivyo haikuwa na maana yoyote kwao kumfuata eneo hilo.
No comments:
Post a Comment