Spika Anne Makinda (kushoto) na Ludovick Utouh. |
Wakati utata wa suala la kodi ya simu ya Sh 1,000
ukitarajiwa kumalizwa katika Bunge lijalo, Spika wa Bunge, Anne Makinda
na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh
wametetea kodi hiyo.
Viongozi hao walitoa kauli za kutetea kodi hiyo, walipozungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti jana, mjini hapa, baada ya ufunguzi wa semina ya siku nne kwa wabunge wa kamati zinazohusu mahesabu ya Serikali.
Wabunge hao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), Kamati ya Hesabu za Serikali za
"Naomba niwe mkweli, suala hilo ni sheria kamili na ilipitishwa bungeni, kamati ya bajeti ni shirikishi, tuwe wakweli, hakuna mtu ananunua simu kwa Sh 3, tumwogope Mungu, kila mtu anapaswa kuchangia maendeleo ya nchi yake, labda awe mgonjwa kabisa asiyeweza kufanya chochote," alisema Spika Makinda.
Makinda alisema Tanzania ikiendelea kujiendesha kwa mtindo wa kila mtu kuona uchungu wa kuchangia maendeleo, hakutakuwa na maendeleo.
"Tutapata wapi maji, barabara na huduma nzuri za afya? Binafsi natamani ifike mahali kila mtu, tukubali tutoe Sh moja tu, tuanzishe Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, maana hakuna asiyejua tatizo la ajira nchini, tuulizane ukweli wa hili, anayeshindwa kupata Sh 1,000 kwa mwezi ni nani? Tusiendekeze hii ni sheria," alisisitiza Makinda.
Kuhusu suala hilo la kodi ya laini, CAG alisema sheria ya kodi inataka kila mapato yanayopatikana, yalipiwe kodi na kama mtu halipi ni kosa. Aidha, alisisitiza wananchi kupenda kuchangia maendeleo yao kwa kuwa hakuna mtu atakayewasaidia kutoka nje.
"Usipolipa kodi ni kosa, tatizo tulilonalo ni mfumo ambao haujawekwa vizuri kukusanya hizo kodi, sidhani kama Sh 1,000 ni tatizo, wanasema watu hawawezi, kodi yoyote inalipwa na watu, ulipaji wa kodi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa, tatizo kubwa ni usimamizi wa utekelezaji wa kinachopatikana," alisema Utouh.
Alisema nchi zingine, akitolea mfano wa Kenya, utamaduni wa kulipa kodi umekua na kuimarika, kiasi kwamba wananchi wanajivunia nchi na maendeleo yao.
Hilo pia lilisemwa na Spika Makinda alipozungumzia utamaduni wa kulipa kodi kwa wananchi kama sehemu ya kuchangia maendeleo yao na Taifa zima.
Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 ndiyo inazungumzia suala la tozo kwa laini za simu ya Sh 1,000 kuanzia mwaka huu wa fedha.
Katika hilo, Makinda hakusita kueleza kuwa anaona huenda tatizo kwa wananchi ni kutoona matumizi ya kodi wanazokatwa, ndiyo maana pengine wanakuwa na wasiwasi.
Hata hivyo, alisema marekebisho ya sheria yatapelekwa bungeni lakini alisisitiza, kuwa Watanzania wanapaswa kubadili mtazamo kuhusu dhana ya kuchangia maendeleo.
Akisisitiza alichosema Makinda na CAG, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, alitaka mamlaka zinazosimamia na kukusanya kodi, kujenga utamaduni wa uadilifu na kuwezesha wananchi kuona matokeo ya kodi wanazokatwa.
"Kuna watu wanadhihirisha kuwa ukifanya kazi mahali fulani mfano TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) umeula, wanaona mtu kaanza kazi jana, leo anamiliki hoteli kubwa; ni tajiri mkubwa wakati ni taasisi ya umma kama nyingine hili si kweli, ni uadilifu tu unahitajika kwa wakusanyaji kodi, ni vizuri tukajenga tabia ya kulipa kodi, nchi za wenzetu kila kitu wanalipia," alisisitiza Kipozi.
Baada ya wanasiasa na asasi za jamii, wakiwamo wabunge waliopitisha kodi hiyo kuipinga nje ya Bunge, Rais Jakaya Kikwete, aliagiza Serikali kukutana na wadau wa simu, kujadili pengo la mapato ya Serikali, ambalo lingetokana na kufutwa kwa kodi hiyo.
Siku chache baadaye, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, waligomea tozo hiyo wakidai hawakushirikishwa katika mchakato wa sheria hivyo hawakubaliani na suala hilo.
No comments:
Post a Comment