Tuesday, August 6, 2013

JOHN TENDWA ASTAAFU RASMI USAJILI WA VYAMA VYA SIASA...

John Tendwa.
Baada ya misukosuko ya kisiasa ya hapa na pale na hasa kulalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa nchini, hatimaye Msajili wa Vyama hivyo, John Tendwa amestaafu utumishi wa umma.

Nafasi yake imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi aliyeteuliwa jana na Rais Jakaya Kikwete kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Jaji Mutungi anakuwa Msajili wa Vyama vya Siasa wa tatu tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, nafasi hiyo ilipochukuliwa kwa mara ya kwanza na George Liundi.
Kutokana na uteuzi huo, baadhi ya wadau wa siasa wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa nchini, wamempongeza Rais Kikwete kwa kumteua Jaji Mutungi na kumtaka aendeleze mema ya Tendwa na kusimamia sheria ipasavyo, bila kupendelea.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam ilieleza kuwa, uteuzi huo ulianza Agosti 2.
Kwa mujibu wa taarifa, kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.
Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na chama tawala, katika pongezi zao kwa Rais Kikwete, walielezea matumaini yao, kwamba uteuzi huo utaleta mabadiliko kutokana na uzoefu wa masuala ya sheria na kanuni alionao Jaji Mutungi.
Akizungumza na mwandishi jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema chama chao hakina neno la kusema kuhusu Tendwa wala Jaji Mutungi kwa kuwa wote wanapaswa kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
"Hatuna maneno ya kusema ikiwa tu anafuata kanuni na sheria zake za kazi kama mtangulizi wake, tumwache afike ofisini, mpeni muda afanye kazi," alisema Nape.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisifu uwezo wa Jaji Mutungi katika masuala ya sheria kwa kupitia kazi kubwa alizofanya akiwa Msajili wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, pamoja na kuwa Jaji, hivyo alimtaka asimamie sheria na kanuni za usajili wa vyama vya siasa ipasavyo.
Hata hivyo, alisema yapo mambo mazuri yaliyofanywa na wasajili waliomtangulia, Liundi na Tendwa  na kumtaka aendeleze mazuri hayo huku akitumia kanuni na sheria kusimamia vyama vya siasa.
"Amefanya kazi kubwa akiwa katika mfumo wa Mahakama, lakini waliomtangulia kuna kazi nzuri wamefanya, achukue kazi nzuri na kuzidumisha.
"Jaji Mutungi ninavyomfahamu, ni mtu wa kanuni, tumwache afike ofisini, atulie na akitushirikisha wadau, tutampa mambo tunayodhani kwetu ni vipaumbele, ayafanyie kazi," alisema Mbatia.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema alisema: "Namkaribisha Jaji Mutungi sana, nimemfahamu kwa karibu katika shughuli za kimahakama, ni mtu mzuri mwenye hekima katika kutenda, tunatarajia atatusaidia katika usajili wa vyama.
"Siwezi kulia kwa Tendwa kuondoka, kwa kuwa alinitesa sana, kidogo afute TLP, najua alikuwa anafanya kazi yake, lakini ulikuwa wakati mgumu, nampongeza Rais Kikwete, namwomba Jaji Mutungi kwa namna alivyo mjuzi wa sheria, afuate sheria ya vyama vya siasa, naamini hatapendelea kwamba kuna chama dume, hilo linatugawa."
Mrema alimshauri Jaji Mutungi kupigania haki ya vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu, vipate ruzuku bila kujali vina wabunge au la, kwa kile alichodai kitasaidia kuwa na ushindani katika uchaguzi na uendeshaji wa masuala ya kisiasa nchini.
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Abdul Kambaya, akizungumza kwa niaba ya chama hicho alisema hawawezi kujua Jaji Mutungi atakuwa mtu wa namna gani kwa nafasi aliyopewa na Rais Kikwete na kumtaka aweke uzalendo mbele, itikadi za kisiasa baadaye.
Akitolea mfano wa uongozi wa Tendwa, Kambaya alidai yapo baadhi ya maeneo Msajili huyo mstaafu alionesha udhaifu wa kutovichukulia hatua kali baadhi ya vyama vilivyosababisha vurugu.
Alitoa mfano wa vurugu kwa kutuhumu CCM na Chadema, kwamba vilihusika katika ugomvi wa wazi katika baadhi ya matukio ikiwamo kampeni kadhaa.
"Hatukuona hatua kubwa za kinidhamu alizochukua Tendwa kushughulikia vyama vya upinzani na CCM kwa vurugu vilizosababisha, maonyo hayakuwa na nguvu na inawezekana ni kutokana na sheria kutompa meno ya kuchukua hatua kali.
"Kama ndivyo, huyu mpya apeleke mapendekezo bungeni kupitia Wizara mama ya Sheria, ili marekebisho yafanyike," alisisitiza Kambaya.
Alidai matukio ya kukatana mapanga katika baadhi ya mikutano ya kisiasa yalitokea waziwazi kwa CCM na Chadema, huku akishutumu baadhi ya wabunge wa vyama hivyo kutumia silaha kama bastola hadharani, bila hatua za kinidhamu kuchukuliwa.
Kwa upande wa Chadema, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche alidai Tendwa aliwahi kutishia kuifuta Chadema, hivyo wanamtakia kila la kheri katika kustaafu kwake na kumtaka Jaji Mutungi kuzingatia miongozo, sheria, taratibu na kanuni za vyama vya siasa.
"Tunamtaka Jaji Mutungi atekeleze kazi zake kwa mujibu wa sheria, miongozo, utaratibu na kanuni zilizopo, sheria zipo wazi kuhusu vyama vya siasa ukianzia na ile ya mwaka 1992, Tendwa aligeuka kiranja wa kututisha kuwa ataifuta Chadema na si CCM," alilalama Heche.
Katika tamko rasmi la Chadema lililotumwa kwa vyombo vya habari kuhusu kustaafu kwa Tendwa, chama hicho kilidai kuwa katika miezi ya mwisho akiwa madarakani, Tendwa aliharibu demokrasia.
Chadema ilidai zaidi kwamba kilikuwa kikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa lakini badala ya kuifuta Chadema kama alivyodai, ameondoka yeye.
Kuhusu uteuzi mpya, chama hicho kilieleza kuwa: "Wapenda demokrasia na maendeleo nchini, wanamtarajia atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na utawala bora, asije akapita njia ya Tendwa."

No comments: