Mzozo wa kodi ya laini za simu, unaotarajiwa kumalizwa katika mkutano ujao wa Bunge, umefikia mwisho Zanzibar, baada ya wawakilishi kuikataa rasmi.
Kabla ya kukataliwa na wawakilishi hao jana, Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma (CCM), aliitaka Serikali ieleze kama Zanzibar ilishirikishwa wakati wa kuamua kodi hiyo itozwe.
"Wenzetu Bara wamepitisha mswada wa tozo la kodi ya simu, sasa nataka kumwuliza Waziri wa Fedha kama Zanzibar imeshirikishwa katika mchakato wa mswada huo," alihoji Hamza.
Alisema alitoa taarifa hiyo mapema kwa Waziri, kuhusu nia ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuongeza kodi ya laini ya simu kwa Sh 1,000.
Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma (CUF), alisema kodi hiyo haitatekelezwa Zanzibar na kushauri mwisho wake iwe katika kisiwa kidogo cha Chumbe, karibu na pwani ya mji wa Zanzibar kutoka Tanzania Bara.
"Nashauri kodi hii mwisho wake iwe kisiwa cha Chumbe kabla ya kuingia Unguja kwa sababu haina maslahi kwa wananchi wa Zanzibar...mimi niko tayari kuandamana kupinga kodi hiyo na wananchi wa jimbo langu," alisema.
Mwakilishi wa Uzini, Mohamed Raza Dharamsi (CCM), alitaka kujua athari za kodi hiyo ya Sh 1,000 kwa wamiliki wa laini za simu kwa mwezi, pamoja na faida zake kwa wananchi wa Zanzibar.
Raza alisema wananchi wengi wanaomiliki simu, ni wanyonge wanaoishi vijijini na hawana uwezo wa kulipia huduma hiyo kwa mwezi.
"Nataka kujua athari za kodi ya simu ya Sh 1,000 kwa mwezi na vipi Zanzibar imeshirikishwa katika mpango huo kodi hii iondolewe haraka," alisema.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ilipanga kuingiza Sh bilioni 178 kutokana na kodi hiyo, ambayo imepangwa kutumika kupeleka umeme vijijini.
Hata hivyo, baada ya kodi hiyo kukubaliwa kisheria katika Bunge lililopita, mjadala wa kuipinga uliibuliwa katikati ya jamii na kusababisha Rais Jakaya Kikwete, kuagiza Serikali ikae na wadau wa simu, zikiwamo kampuni za simu, kumaliza mzozo huo.
Katika vikao hivyo, Waziri wa Fedha, William Mgimwa, alisema lengo ni kujadili vyanzo vingine vya kupata Sh bilioni 178, ambazo zilitarajiwa kupatikana katika kodi hiyo, kama itakubaliwa kufutwa.
Mgimwa alisema baada ya kukubaliana kuhusu vyanzo hivyo vipya, mzozo huo utahamia bungeni ambako utamalizwa kisheria, baada ya kukubaliana vyanzo mbadala vya kufidia pengo hilo.
Akijibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alisema Zanzibar haijashirikishwa katika suala la kodi ya laini za simu.
Alisema suala la simu na mawasiliano ni la Muungano, lakini kwa bahati mbaya Zanzibar haijashirikishwa katika uamuzi wa suala hilo.
"Kwa bahati mbaya nimeulizwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakitaka kujua Zanzibar imeshirikishwa vipi katika suala la kodi ya laini za simu...kweli mimi sijashirikishwa," alisema.
No comments:
Post a Comment