CHADEMA WAENDELEA KUKALIA USHAHIDI WA BOMU LA ARUSHA...

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kukalia ushahidi kinaodai kinao kuhusu mlipuko wa bomu uliotokea mwezi uliopita kwenye mkutano wa chama hicho wa kuhitimisha kampeni za udiwani mkoani Arusha. 

Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Freeman Mbowe amesema hawautoi hadi hapo Rais Jakaya Kikwete atakapounda tume huru ya kimahakama.
Alisema muda ukifika, ushahidi huo utawekwa wazi kwa wananchi, vyama na mashirika ya kiraia ya haki za binadamu nchini na nje ya nchi.
Pia kimesema kitaupeleka ofisi za kibalozi za mataifa rafiki na Tanzania pamoja na jumuiya za kimataifa ili yashinikize tume huru iundwe.
Mbowe alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa kikao cha dharura  cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika Dar es Salaam. 
Katika hatua nyingine, Chadema imesema itaanzisha makambi ya vijana nchini, watakaotumika kuhakikisha usalama katika mikutano yao na kuwalinda viongozi wao.
Kuhusu Rasimu ya Katiba , alisema Kamati Kuu imepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu hiyo.

No comments: