Meno ya tembo. |
Ofisa Uvuvi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT ), Seleman Chasama (50), amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na meno ya tembo, yenye thamani ya Sh bilioni 4.2.
Chasama alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwasebo.
Alisomewa mashitaka hayo chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mshitakiwa akipatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 15 au adhabu nyingine ikiwemo kulipa faini.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili Kimaro alidai kuwa Julai 4 mwaka huu katika eneo la Mbezi Makabwe Kinondoni Dar es Salaam, Chasama alikamatwa akiwa na nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo 347, yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 2.6 sawa na Sh bilioni 4.2.
Mshitakiwa hakutakiwa kujibu mashitaka, kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na mshitakiwa alirudishwa rumande hadi Julai 24 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment