Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. |
Moto mkubwa ulioteketeza zaidi ya ekari 40 za msitu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro haujaathiri shughuli za watalii kupanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.
Aidha hakuna wageni walioahirisha safari za kupanda mlima huo, huku juhudi kubwa zikifanyika kuudhibiti moto huo.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Pascal Shelutete alisema hadi kufikia jana jioni zaidi ya asilimia 75 ya moto ulikuwa umedhibitiwa.
“Shughuli za Utalii katika Mlima Kilimanjaro zinaendelea kama kawaida, hakuna watalii walioathirika na moto, hasa kwa njia zote muhimu za Marangu, Mweka, Machame, Umbwe, Lemosho na Rongai zinazotumika kwa ajili ya kupandisha watalii mlimani na zile za kushukia hazijaathiriwa na moto,” alisema.
Shelutete pia alisema Hifadhi ya Kilimanjaro(KINAPA) imeweka kambi mbili maalumu kwa ajili ya kuhudumia wanaoshiriki zoezi la kuzima moto moja ikiwa katika eneo la Nanjara wilayani Rombo na nyingine eneo la Marangu.
Moto katika mlima huo ulianza Julai saba, katika maeneo ya Amboni, Ushiri, Keryo, Kimori na Shimbi wilayani Rombo na inasadikiwa ulisababishwa na warina asali.
No comments:
Post a Comment