Thursday, June 13, 2013

MWILI WA MZEE APIYO KUWASILI LEO KUTOKA AFRIKA KUSINI...

Mzee Timothy Apiyo.
Mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Timoth Apiyo, unatarajiwa kuwasili leo nchini ukitokea Afrika Kusini na utapokewa na Makatibu Wakuu wastaafu na viongozi wengine waandamizi wa serikali.
Apiyo alifariki dunia juzi usiku katika hospitali ya Millpark jijini Johanesburg na mwili wake utawasili katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere leo saa 8.00 mchana.
Msemaji wa familia ya marehemu, Baraka Dinda, alisema mara baada ya mwili huo kuwasili utapokelewa na Makatibu wakuu wastaafu ambao ni John Rupia, Philemon Luhanjo na Katibu Mkuu Kiongozi wa sasa Ombeni Sefue.
Alisema mwili huo ukiwasili nchini utapelekwa nyumbani kwa marehemu maeneo ya Segerea Ukonga, jijini Dar es Salaam na keshokutwa utasafirishwa kwenda kijijini kwake Marasibora, Rorya mkoani Mara kwa mazishi.
Dinda alisema shughuli zote za kusafirisha mwili huo hadi maziko zinafanywa na Serikali huku kukiwa na mpango wa kufanya ibada mbili nyumbani kwa marehemu na katika viwanja vya Karimjee.
Akimzungumzia marehemu Apiyo, aliyewahi kuwa Waziri wa Afya na Mbunge Rorya, Profesa Philemon Sarungi ambaye anakiri mafanikio yake katika utendaji yamechangiwa na ushauri aliokuwa akipata kutoka kwa marehemu na kusema anajivunia kwa uadilifu na utendaji kazi wa msomi huyo wa kwanza katika wilaya ya Rorya.
Alisema ili kumuenzi ni vema kudumisha uadilifu bila kuwa na kiburi kwa viongozi, kusikiliza shida za watu hususan wa chini kwa kuwa kiongozi ni mtumishi wa watu kwa vitendo na si kuwa mtawala ambaye ni dikteta.
Apiyo alizaliwa katika wilaya ya Rorya, Tarafa ya Suba, mkoani Mara na kupata  elimu ya msingi na sekondari akiwa hapo na mwaka 1959 alijiunga na Chuo Kikuu cha East Afrika na kuchukua shahada  ya kilimo. Alijiendeleza kwa masomo katika vyuo vikuu kadhaa nje ya nchi na kisha kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali.
Aprili 1974, Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere alimteua kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Julai 1986 alistaafu kazi.

No comments: