Friday, June 14, 2013

BAJETI YANG'ATA NA KUPULIZA, WANYWAJI NA WAVUTAJI KILIO...

Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa akionesha mkoba wake wenye Bajeti ya Serikali Dodoma jana.
Ni bajeti inayong’ata na kupoza machungu kwa wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara nchini.
Pengine ndivyo inavyoweza kuzungumzwa hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2013/14 iliyosomwa bungeni jana na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa.
Akisoma hotuba hiyo, Waziri Mgimwa alisema  Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 ili kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 14 hadi asilimia 13.
"Kutoa msamaha wa VAT kwa wazalishaji wa nguo nchini zinazozalishwa kwa pamba  ya ndani kwa bidhaa na huduma zitakazotumika tu kwenye uzalishaji wa nguo hizo.
"Kwa hatua hii mzalishaji wa nguo zinazotumia pamba ya nchini hatalipa VAT kwenye ununuzi wake katika uzalishaji wa nguzo hizo," alisema.
Waziri Mgimwa alisema ili kuongeza uwezo wa serikali kugharimia miundombinu ya barabara imependekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa mafuta ya petroli.
"Kuongeza kiwango cha ushuru wa mafuta kutoka Sh 200 kwa lita hadi Sh 263 kwa lita sawa na ongezeko la Sh 63 kwa lita. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh milioni 155,893.50," alisema.
Pia alipendekeza kupunguza tozo ya kuendelea na mafunzo ya ufundi stadi (SDL) kutoka kwenye kiwango cha sasa cha asilimia 6 hadi asilimia 5 sambamba na kupunguza kiwango cha sasa cha SDL.
"Taasisi za Serikali zisizotegemea bajeti ya Serikali kwa kiwango kikubwa katika kujiendesha pia zitalipa kodi hii," alisema.
Pia Waziri Mgimwa alipendekeza kufanya marekebisho ya sheria ya usalama barabarani ili kuongeza viwango vya ada ya mwaka ya leseni za magari.
Alisema gari lenye ujazo wa injini 501cc-1500cc kutoka kiwango cha sasa Sh 100,000 hadi Sh 200,000; gari lenye ujazo wa injini 1501cc-2500cc kutoka kiwango cha sasa Sh 150,000 hadi Sh 200,000, wakati gari lenye ujazo wa injini ya zaidi ya 2501cc  kutoka kwango cha sasa Sh 200,000 hadi Sh 250,000.
Alisema magari yenye ujazo wa injini chini ya 501cc hayatatozwa ada ya leseni za magari."Bajaji na bodaboda hakuna ushuru... tuwaache vijana wetu wafanye kazi," alisema Waziri Mgimwa na kucheka.
Pia alisema ili kutekeleza dhamira ya serikali ya kusambaza umeme vijijini alipendekeza kuanzisha tozo ya mafuta ya petoli ya Sh 50 kwa lita ambayo itakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
"Mapato yatakayokusanywa kutoka kwenye tozo hii yatatumika kugharimia mahitaji ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika kusambaza umeme vijijini," alisema na kuongeza kuwa hatua hizo za kodi zitaanza kutozwa Julai mosi isipokuwa itakapotangazwa vinginevyo.
Katika kung’ata na kupuliza kidogo, Serikali imekubali kuongeza fedha katika sekta za maendeleo nchini huku pia ikipandisha kodi kwa baadhi ya bidhaa na huduma ili kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Katika hatua hiyo, Serikali imetangaza hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza kodi ya mafuta jami ya petroli isipokuwa mafuta ya taa ambayo yanatumiwa zaidi na wqananchi wa kipato cha chini.
Kwa mujibu wa bajeti ya Serikali iliyosowa jana na Waziri wa Fedha, Wikliam Mgimwa, mafuta ya dizeli yanapanda kutoka kiwango cha sasa cha Sh 215 kwa lita hadi Sh 217 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi mbili.
Petroli inapanda kutoka kiwango cha sasa cha Sh 339 kwa lita hadi Sh 400 kwa lita; huku mafuta ya taa kiwango cha sasa cha Sh 400.30 kwa lita kikiendelea kama kilivyo.
Imepandisha kodi katika vinywaji mbalimbali; baridi, mvinyo, pombe, vinywaji vikali, sigara n.k. kwa asilimia 10 ambapo vinywaji baridi, kutoka Sh 83 kwa lita hadi Sh 91 kwa lita; ongezeko la Sh 8 kwa lita.
Maji ya matunda yaliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa nchini yanapanda kutoka Sh nane kwa lita hadi Sh tisa 9 sawa na ongezeko la Sh moja; huku juisi iliyotengenezwa kwa matunda yasiyozalishwa nchini ikipanda kutoka Sh 100 hadi Sh 110 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh 10.
Kuhusu bia inayotengenezwa kwa nafaka ya nchini na ambayo haijaoteshwa, inapanda kutoka Sh 310 hadi Sh 341 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh 31 huku bia zingine zote, zikipanda kutoka Sh 525 hadi Sh  578 kwa lita; yaani ongezeko la Sh 51.
Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu za ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, unapanda kutoka Sh 145 hadi Sh 160 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh 15 kwa lita moja wa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, unapanda kutoka Sh 1,614 kwa lita hadi Sh 1,775 kwa lita. Sawa na ongezeko la Sh 161.
Kuhusu vinywaji vikali, vinapanda kutoka Sh 2,392 hadi Sh 2,631 kwa lita; sawa na ongezeko la Sh 239; lakini waziri Mgimwa valisema kwa maji yanayozalishwa nchini ushuru hautaongezwa hivyo bei kubaki pale pale.
Akizungumzia sigara, alisema zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku ya nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, zinapanda kutoka Sh 8,210 hadi Sh 9,031 kwa sigara 1,000; sawa na ongezeko la senti 82 kwa sigara.
Zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka Sh 19,410 hadi Sh 21,351 kwa sigara 1,000; likiwa ni ongezeko la Sh moja na senti 94 kwa sigara.
Sigara nyingine zenye sifa tofauti na zilizotajwa juu zinapanda kutoka Sh 35,117 hadi Sh 38,628 kwa sigara 1,000; ikiwa ni ongezeko la Sh tatu na senti 50 tu kwa sigara moja;
Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara inapanda kutoka Sh 17,736 hadi Sh 19,510 kwa kilo; na ushuru wa bidhaa kwa biri (cigar) unabaki kuwa asilimia 30.
Hatua hizi kwa mujibu wa Waziri Mgimwa zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh milioni 510,017.50.

No comments: