Tuesday, February 5, 2013

MUDA WA KUTOA MAONI YA KATIBA WAMALIZIKA...

Jaji Joseph Warioba.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imekamilisha rasmi kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, makundi maalumu na watu mashuhuri.
Kukamilika kwa kazi hiyo, kumetoa nafasi kwa Tume kuanza uchambuzi wa maoni hayo yote na kuandaa Rasimu ya Katiba inayotarajiwa kukamilika Mei mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alisema baada ya rasimu hiyo kukamilika, itawasilishwa katika mikutano ya mabaraza ya Katiba itakayoanza Juni.
“Tume imemaliza kukusanya maoni binafsi ya wananchi, kukutana na makundi maalumu … imekamilisha kazi ya ukusanyaji maoni,” alisisitiza Warioba.
Alisema wakati Tume ilipokutana na makundi maalumu kuanzia Januari 7 hadi 28, ilikutana na vyama vya siasa 19, taasisi za kidini 22, asasi za kiraia 72, taasisi za kiserikali 71 na viongozi na watu mashuhuri kutoka Bara na Zanzibar.
Alisema rasimu ya Katiba itakayoandaliwa, itachapishwa katika magazeti kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 inavyoelekeza.
Alifafanua kuwa lengo ni kutoa fursa kwa wananchi  kuisoma kabla ya kuwasilishwa rasmi katika mabaraza ya Katiba yatakayoitishwa na Tume nchini kote.
Alisema mchakato wa kuunda mabaraza utaanza Juni na wajumbe wa mabaraza hayo, watachaguliwa na wananchi kuanzia ngazi ya Kijiji.
Kazi yao kubwa kwa mujibu wa Jaji Warioba, itakuwa kuwakilisha maoni ya wananchi katika mikutano ya mabaraza hayo.
“Kwa sasa Tume imekamilisha mwongozo wa namna bora na ya kidemokrasia ya kupata wajumbe wa mabaraza hayo ambao utasambazwa nchini kote na tayari umetangazwa katika vyombo vya habari, ili wananchi waufahamu na kuutolea maoni,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa mwongozo huo, katika mikoa ya Bara mbali na Dar es Salaam, kila kata itawakilishwa na wajumbe wanne watakaoungana na madiwani wa kata na wa viti maalumu katika Baraza la Katiba la Wilaya.
Jaji Warioba alisema kwa Dar es Salaam, Tume imeandaa utaratibu tofauti wa kupata wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya Wilaya, ambapo kila kata watatoka wajumbe wanane watakaoungana na madiwani wa kata na wa viti maalumu.
“Kwa msingi huo, kutakuwa na wajumbe 18,169 watakaohudhuria mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa Bara wakati Zanzibar wajumbe wa mabaraza ya Katiba kwa ujumla watakuwa 1,198,” alisema.
Akizungumzia upande wa Zanzibar, Mwenyekiti huyo alisema kutakuwa na mabaraza ya wilaya ngazi ya mamlaka ya Serikali za mitaa 13, ambapo kila shehia itawakilishwa na wajumbe watatu watakaoungana na madiwani wa wadi, viti maalumu na wa kuteuliwa walio kazini kwa sasa.
Alisema sifa za waomba nafasi ya ujumbe wa mabaraza hayo ya Katiba ya wilaya ni kuwa raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 na zaidi.
Mjumbe pia anapaswa awe na uwezo wa kusoma na kuandika, mkazi wa kudumu wa kijiji/mtaa/shehia husika, mtu mwenye hekima, busara na uadilifu.
“Wananchi wanaopenda kuwa wajumbe wa mabaraza haya, watatakiwa kuwasilisha majina yao kwa maofisa watendaji wa vijiji/mtaa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar, watawasilisha kwa sheha katika tarehe itakayoelezwa na Tume baadaye,” alifafanua Warioba.
Alisema wajumbe wa mabaraza hayo watakapopatikana, watakuwa na jukumu la kujadili rasimu ya Katiba, itakayowasilishwa na Tume kabla ya rasimu hiyo kuwasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba ili kujadiliwa.

No comments: