![]() |
| Mandhari ya Kisiwa cha Ukerewe. |
Baada
ya Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (Chadema), kuliambia Bunge kuwapo kwa
askari wa Kenya na Uganda kinyemela kisiwani Ukerewe na kuhatarisha amani zipo
taarifa kuwa hao ni maofisa uvuvi wa Afrika Mashariki.
Imeelezwa
kuwa maofisa hao wako kisiwani humo wakishirikiana na polisi wa nchini kukamata
nyavu zilizopigwa marufuku kutumiwa ziwani kuvua samaki.
Machemli,
ambaye jana aliomba Mwongozo wa Spika na kupewa nafasi, aliliambia Bunge kuwa
askari hao wa nchi jirani, wamekuwa wakipiga wananchi na kuwadhalilisha kwa
kisingizio cha kudhibiti uvuvi haramu.
Mbunge
huyo alisema askari hao wamekuwa wakidai kutafuta nyavu ndogo, ambazo wanadai
ni haramu kwa shughuli za uvuvi.
Kutokana
na kauli hiyo, Spika Anne Makinda, aliagiza Serikali kutafuta uhakika wa habari
za askari hao wa Kenya na Uganda kuingia kinyemela kisiwani Ukerewe na kutoa
taarifa.
Kauli
hiyo ya Spika ilikuja bungeni jana baada ya Machemli (Chadema), kutoa hoja
bungeni akitaka Bunge lijadili kuhusu kitendo cha askari wa nchi hizo kuingia
nchini kinyemela.
Spika
Makinda alisema Bunge haliwezi kujadili hoja hiyo wakati Serikali haijafanya
uchunguzi wa kutosha kuhusu kuingia kwa askari hao na kuagiza ifanye uchunguzi
kuhusu suala hilo.
Hata
hivyo, taarifa kutoka kwa Mwandishi Jovither Kaijage, aliye Ukerewe, zilieleza kuwa hakuna uvamizi wa
aina hiyo, isipokuwa ni operesheni dhidi ya uvuvi haramu, inayotekelezwa na
maofisa uvuvi wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Inadaiwa
maofisa hao wakisaidiwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), wamevunja nyumba na kupiga
wananchi kwa kisingizio cha kutafuta zana haramu za uvuvi.
Habari kutoka kata
za Ngoma, Bwiru na Ilangala zilisema kabla ya
uperesheni hiyo kufanyika katika maeneo hayo, polisi walipiga risasi
angani na kufyatua mabomu ya kutoa machozi.
Hali
hiyo ilizua taharuki na kusababisha watu wakimbie ovyo huku
wengine wakikamatwa na kupigwa, wakati huo baadhi ya milango ya
nyumba zao ikivunjwa na maofisa hao kutafuta zana haramu
za uvuvi.
Mmoja
wa wafanyabiashara wa maduka katika mwalo wa Bukimwi, katika
kata ya Ngoma, Ruigi Ghatawa, alidai katika ghasia hizo juzi
mchana, duka lake lilivunjwa na fedha Sh 270,000 kuibwa
na watu hao.
Ofisa
Uvuvi wa Mkoa wa Mwanza, Lameck Mongo, anayeongoza operesheni hiyo ya
siku sita iliyoanza Januari 31, alikanusha tuhuma hizo za kuvunja nyumba na
kupiga watu.
Hata
hivyo, alikiri kuwa polisi walitumia mabomu kutawanya wananchi ili
wasidhuru maofisa hao wa doria na kuongeza kuwa wavuvi wanaonyang’anywa zana
hizo haramu, ndio wanatoa taarifa hizo za uzushi ili waonekane wanaonewa.
Alisema
wao hawakwenda Ukerewe kuonea watu, ila wanatafuta wahalifu na
kuongeza kuwa ni lazima zana hizo zitafutwe na kuharibiwa.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, mbali ya kuahidi kufuatilia ili
kupata ukweli wa suala hilo, pia alisema hajapata taarifa hizo na
kuongeza kuwa operesheni hiyo inatekelezwa chini
ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya na ndiye anatakiwa kuulizwa suala
hilo.
Mkuu
wa Wilaya, Mary Tesha alipoulizwa , alipuuza madai hayo ya
wananchi na kuongeza kuwa
hivyo ni visingizio baada ya zana haramu
walizokuwa wakimiliki kukamatwa na kuharibiwa.
No comments:
Post a Comment