![]() |
| Askofu Thomas Laizer. |
Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, amemtembelea na kumjulia hali Askofu Thomas Laizer wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati,
aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Selian jijini hapa.
Pinda
alikwenda hospitalini hapo jana saa 9 alasiri na kukaa zaidi ya nusu saa, huku
waandishi wa habari wakizuiwa kuingia katika chumba alimolazwa cha wagonjwa
wanaohitaji uangalizi maalumu.
Hata
hivyo, baada ya kutoka katika chumba hicho kama ilivyo ada ya viongozi
kuzungumzia hali ya mgonjwa, Pinda hakuzungumza na waandishi wa habari na
kulikuwa na ulinzi mkali ambapo pia waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza
naye.
Askofu
Laizer amelazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na hakuna daktari wala ndugu
aliye tayari kusema ugonjwa unaomsibu.
Awali
ilisemekana kuwa Askofu Laizer amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC
ya Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya watu wengi kumiminika Selian kutaka
kumwona, lakini jana ilidhihirika kuwa, amelazwa hospitalini hapo.
Mwandishi
alijaribu kuzungumza na watumishi wa
hospitali hiyo, ambao hawakutaka kutajwa majina yao, waliotaka waumini
wamwombee Askofu Laizer.
Kabla
ya Waziri Mkuu Pinda kufika hospitalini hapo, asubuhi alifungua mkutano wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unaoshughulikia masuala ya gesi na
mafuta na mchana alitembelea kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika
mazingira magumu cha SOS, Ngaramtoni,
nje kidogo ya hapa.
Akiwa katika kituo hicho, Pinda alitoa Sh
milioni 20 kusaidia watoto hao na kuomba wadau wengine, wenye uwezo kujitokeza
kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment