Wednesday, February 6, 2013

ASKOFU MALASUSA KUKUTANA NA WACHUNGAJI KKKT LEO...


Askofi Mkuu Alex Malasusa.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Alex Malasusa anatarajia kukutana na wachungaji na wainjilisti wa Jimbo la Arusha Magharibi Dayosisi ya Kaskazini Kati leo makao makuu ya Jimbo hilo Ngaramtoni nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Askofu Malasusa yuko hapa kwa zaidi ya wiki moja sasa na amekuwa akikutana na viongozi wa Kanisa hilo kwa lengo la kujua kiini cha mgogoro wa Dayosisi hiyo uliodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na kufikia hatua ya kuunda Kamati ya Maaskofu sita kuchunguza kiini cha mgogoro huo na kupata mapendekezo ya Kamati hiyo ili kufia hatua ya kutoa uamuzi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Dayosisi hiyo zilisema kuwa kikao hicho kinatarajia kufanyika leo kuanzia saa 4 asubuhi makao makuu ya Jimbo hilo na tayari taarifa za kuwepo kwa kikao hicho zimesambazwa kwa wachungaji wote 13 wa Jimbo hilo.
Habari zilisema kufanyika kwa kikao hicho ni kutaka Askofu Malasusa apate maoni ya wachungaji na wainjilisti wa Jimbo hilo juu ya mgogoro huo.
Usharika wa Ngateu uliopo Jimbo la Arusha Magharibi ndiko chimbuko kubwa la kuibuka kwa mgogoro huo kwani Mchungaji Philemoni Mollel alikuwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo na kufikia hatua ya kufukuzwa kazi na kuzuiwa kufanya kazi za kichungaji ndani ya Kanisa hilo hatua iliyopingwa na washarika wa Usharika huo na kufikia hatua ya kutaka kuandamana hadi makao makuu ya Dayosisi hiyo.
Vyanzo vilisema kuwa taarifa ya kufanyika kwa kikao hicho ilikuwa ikisambazwa jana na juzi na Katibu wa Jimbo aliyetambulika kwa jina moja la Meidamei kwa njia ya ujumbe wa simu za mikononi za wachungaji wa jimbo hilo.
Ujumbe ulisomeka: ‘’Wapendwa wachungaji Shalom! Poleni na kazi. Nawaandikia kuwahimiza wachungaji wote tarehe 6/02/2013 saa 4 asubuhi wote tuwe tumefika jimboni kila mchungaji aje na wainjilisti kama mwaliko uliotangulia wa Katibu wa Jimbo ulivyoelekeza. Kikao hiki ni muhimu sana kwa ajili ya kukutana na ujumbe wa Kanisa (Mkuu wa jimbo),’’ ilimaliza sehemu ya ujumbe huo.
Habari zilisema kabla ya ujio wa Askofu Mkuu wa Kanisa leo  katika Jimbo hilo, Jimbo lilipanga semina kwa wachungaji na wainjilisti hivyo semina hiyo ilifutwa kutokana na ugeni huo.
Ujumbe huo kwa wachungaji ni kutoka kwa Katibu wa Jimbo ulisomeka  ifuatavyo: ‘’Wapendwa naomba niwajulishe kilichosababisha kuahirisha semina ya tarehe 6/02/2013 Jumatano saa 3 asubuhi, wachungaji na wainjilisti wote wanahitajika kuonana na ugeni wa Kanisa wa Dayosisi hiyo, hivyo ugeni huu ni wa watu 155 tunaomba kwa kusaidia mapokezi kila usharika utupe Sh 80,000 (kasima ya mapato mengine) walio mbali mtume kwa M-pesa na mtakuta risiti zenu. Ahsanteni sana,’’ ilisema sehemu ya ujumbe huo.
Jimbo la Arusha Magharibi lina sharika 13 kutokana na ujumbe huo wa Katibu wa Jimbo wa kutaka kila usharika kuchangia kiasi hicho ni Sh 1,040,000 zitakusanywa iwapo kila usharika utatimiza.  
Wakati huo huo, jana katika shauri lililofunguliwa na Mchungaji Philemon Mollel kupinga kufukuzwa kazi bila ya kufuata taratibu katika Tume ya Usuluhisho ya Idara ya Kazi jijini Arusha dhidi ya Baraza la Wadhamini la Dayosisi ya Kaskazini Kati, uongozi wa Dayosisi hiyo ukiongozwa na wakili wao Israel Mwaluko uliweka pingamizi katika shauri hilo kwa mdomo hatua iliyopingwa na Msuluhishi.
Kutokana na hali hiyo, Msuluhishi wa Tume hiyo alimtaka Wakili Mwaluko kuwasilisha pingamizi hilo kwa maandishi kabla ya Februari 11 na Mchungaji Mollel anapaswa kujibu pingamizi hilo kabla ya Februari 18 na Februari 21 ni mwisho wa kuzipitia pingamizi hizo.

No comments: