Monday, February 4, 2013

BENDERA YA CHADEMA YAZUA BALAA SHEREHE ZA CCM...

Sherehe ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma imevurugwa na kukatishwa na Chadema, kutokana na kuchomeka bendera yao uwanjani katika viwanja vya baa ya Mwanga mjini hapa jana wakati zinaendelea.
Sherehe hizo zilizoshirikisha wanaCCM wa kata  tatu za Majengo, Mji Mpya na Viwandani pamoja na wabunge, mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine, viongozi wa Chadema walikwenda kusimika bendera yao katikati ya bendera za CCM na kusababisha vurugu kubwa.
Kwa dakika 30 hivi, sherehe hizo zilivurugika huku wafuasi wa CCM na wabunge akiwamo Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), walitoka jukwaani na kuanza kupambana na wafuasi wa Chadema waliokuwa wakichomeka bendera yao na kuanza kunyang’anyana.
Wafuasi wa CCM na wabunge walifaulu kunyang’anya bendera hiyo na kuwafukuza wafuasi wa Chadema na kuwakimbiza nje ya viwanja hivyo. Jeshi la Polisi lilifika uwanjani hapo na kuanza kutuliza vurugu hizo huku wakiwasaka wafuasi wa Chadema na kuwakamata wawili na kuwapeleka kituoni.
Polisi waliongeza askari waendesha pikipiki, waliozunguka eneo hilo huku wafuasi wa CCM waliosambaa hapo, hawakuendelea na hotuba wala matangazo, badala yake waliweka muziki na kuserebuka.
Kutokana na vurugu hizo, eneo hilo lilikuwa limejaa askari wakizunguka kwenye gari na pikipiki. Wafuasi wa CCM waliondoa bendera zao na kuondoka kwa makundi na mkutano ukaisha kwa mtindo huo.
Dalili za kuzuka vurugu uwanjani hapo, zilijitokeza tangu mapema asubuhi kabla ya kuanza sherehe hizo kwa maandamano, kutokana na wafuasi wa Chadema, kulalamika kwamba bendera yao iliyokuwa katika eneo hilo la wazi kwa muda mrefu, imeondolewa na kusimikwa za CCM.
Wafuasi hao waliilalamikia Polisi hadi kwenda Kituo cha Polisi cha Mji Mpya kutafuta suluhu, wakitaka bendera yao isimikwe wakati sherehe za CCM zinaendelea uwanjani hapo.
Eneo hilo la wazi linatumika kwa kuegesha pikipiki, bodaboda na magari, linamilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), limekuwa likitumika kwa mikutano na sherehe mbalimbali.
Kabla ya kuvunjika sherehe hizo, mgeni rasmi, Mbunge, Nyangwine, akiwahutubia wanaCCM alisema wakati umefika vyama vya upinzani kuachana na vurugu kwani hazina tija kwa taifa.
Mbunge wa Njombe Kaskazini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga aliwataka wapinzani wabadili kauli ya kusema CCM haijafanya kitu wakati Dodoma sasa inang’aa kwa barabara.
Rage aliwataka wafuasi wa vyama nchini kutunza amani na wajifunze kutoka kwa Algeria na Misri, ambazo wananchi wake wanajuta kufanya mapinduzi, yaliyoporomosha uchumi wao na sasa wanaishi kwa tabu.

No comments: