![]() |
| Marehemu Askofu Thomas Laizer. |
Askofu Dk Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati Arusha amefariki dunia jana alasiri katika Hospitali ya Rufaa ya Selian iliyopo jijini Arusha.
Hospitali hiyo inamilikiwa na kanisa hilo.
Askofu Laizer juzi alitembelewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alitumia zaidi ya nusu saa ndani ya chumba cha uangalizi maalumu (ICU) alichokuwemo askofu huyo.
Habari za uhakika kutoka kwa madaktari waliokaribu na marehemu, ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao walikiri kutokea kwa kifo cha Askofu huyo na kueleza kuwa uongozi mzima wa dayosisi hiyo ulikuwa hospitalini hapo majira ya alasiri mpaka jioni.
Askofu Laizer inadaiwa alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa figo na mapafu ambapo alilazwa katika hospitali hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja huku akiruhusiwa na kurudishwa kutokana na hali yake kuwa tete mpaka mauti yalipomfika.
Habari zilisema uongozi wa dayosisi leo unatarajia kutoa taarifa juu ya kilichosababisha Askofu huyo kufariki na taratibu za mazishi zitakavyokuwa.
Askofu huyo amefariki wakati dayosisi hiyo ikiwa na mgogoro mkubwa katika usharika wa Ngateu Jimbo la Arusha Magharibi kufuatia usharika huo kupinga kufukuzwa kazi kwa mchungaji wao kiongozi Philemon Mollel.
Kufuatia mgogoro huo Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Dk Alex Malasusa ameunda Tume ya Maaskofu sita wa nje ya dayosisi kuchunguza mgogoro huo.

No comments:
Post a Comment