Friday, February 8, 2013

JAMES MBATIA AGOMA KUJIUZULU UBUNGE...

James Mbatia.

Bunge limethibitisha kwamba mitaala ya elimu iliyowasilishwa na Serikali bungeni, ni halali na haijachakachuliwa.
Mitaala hiyo iliwasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk  Shukuru Kawambwa baada ya kuombwa na Bunge wiki iliyopita kuiwasilisha, ili kuhakikisha Serikali inayo.
Akitangaza jana taarifa ya Kamati iliyoundwa na Bunge kuchunguza uhalisi wa mitaala hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema Kamati imepitia na kubaini ni halali na hivyo watagawia wabunge.
Spika Makinda alisema mitaala hiyo iliyowasilishwa na Serikali kama ilivyoombwa na Bunge kufanya hivyo, ilipitiwa na Kamati ya wabunge sita chini ya Mwenyekiti, Margaret Sitta (CCM) na kubaini kuwa haijachakachuliwa.
Spika Makinda alisema, Kamati ilikuwa na hadidu ya rejea moja ya kuthibitisha uhalali, lakini pia ilitumia Sheria ya Elimu ya Mwaka 1975 na nyaraka mbalimbali zikiwamo namba moja na mbili za mwaka 2006.
Wakati wa uchunguzi wa mitaala hiyo, Mbunge wa Kuteuliwa James Mbatia (NCCR-Mageuzi) aliyelalamika kwamba Serikali haina mitaala alikuwamo, wakashirikiana na wataalamu kutoka wizarani kuchunguza kama ni sahihi na inafaa kutumika.
Kabla ya kuundwa Kamati, Mbatia alisema bungeni kama Serikali ingepeleka mitaala hiyo bungeni, angejiuzulu ubunge.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari,  Mbatia  alisema hatajiuzulu kwa madai kuwa mitaala iliyowasilishwa bungeni ni bandia. 
Alisema msingi wa hoja zake ni kwamba mitaala hiyo si rasmi na aliikosoa iliyowasilishwa na Waziri, kwamba haina namba ya International Standard Book (ISBN) na haikusainiwa na mtu yeyote.  Mbatia alisema Kamishna wa Elimu alipaswa kuisaini. 
Alisema mtaala wa sekondari, unataja kuwa ni wa Tanzania Bara badala ya kuwa wa Jamhuri ya Muungano. “Mtaala rasmi wa elimu haujaletwa,” alisema Mbatia akizungumza na waandishi wa habari. 
Kwa upande wake, Waziri Kawambwa, alisema mitaala si machapisho yanayopewa ISBN. 
Alisema ISBN hutolewa kwa maandishi kwa vitabu na Maktaba Kuu ndiyo yenye dhamana ya kuitoa. “Mitaala si kitu kinachopewa ISB namba …mwulizeni Mkuu wa Maktaba kama mitaala inatakiwa kuwa na namba hii,” alisema.
Kuhusu mtaala wa sekondari kuwa wa Bara, Dk Kawambwa alisema yapo mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano.
Alisema Elimu ya Juu ndiyo ya Muungano, lakini ya msingi na sekondari si suala la Muungano.
Alisema kinapotengenezwa chochote kisicho cha Muungano, Zanzibar wana ruhusa kuandaa chao na kutoa mfano wa  elimu ya msingi kwa upande wa Zanzibar, ambayo inaanzia darasa la kwanza hadi kidato cha pili wakati Bara ni hadi darasa la saba.
”Tumekubaliana kuwa kwa upande wa sekondari, mtihani tufanye mmoja tukawaambia tutumie vitabu tunavyotumia pamoja,” alisema. 
“Katika hoja alisema nchi haijawahi kuwa na mitaala tangu uhuru hadi mwaka 2011 tumemhakikishia, tuliyowasilisha ni mitaala rasmi na urasmi wake ni nyaraka zilizoidhinisha kuwa ni rasmi,” alisema. 
Dk Kawambwa aliendelea kusema:“Nimesikitika sana na hata wengine mliniona natetemeka nikawa nasema huyu bwana anajiamini ana kitu gani ambacho mimi sikijui?
“Nilimfananisha na mtu ambaye anataka kujinyonga na ananiomba kamba, nikasita, ananiombaje kamba ajinyonge mwenyewe? Nikaona mwishowe sawa, kama anataka hivyo niwasilishe, nitawasilisha. Na nimewasilisha na Kamati ya Spika imethibitisha
akiwamo yeye.”
Akizungumzia hatua ya Mbatia kulalamika, Waziri alisema katika Kamati alikuwa na nafasi kubwa kama mjumbe kuwasilisha kwenye Kamati mitaala aliyonayo. 
Kwa mujibu wa Waziri, Mbatia alionesha bungeni karatasi ambayo ni bandia akisema ni mitaala. 
“Nikamweleza kama Waziri wa Elimu, kama ana uhakika aiache kwa Spika lakini hakuacha. Kama ni kupanda dau na mimi napanda dau, kama ameacha hiyo karatasi kwa Spika, na mimi najiuzulu uwaziri wangu … akisema ameacha kwa Spika nasisitiza na mimi najiuzulu,” alisema.
Dk Kawambwa alimtaka Mbatia ataje maofisa wa Wizara waliompa taarifa potofu, kwa sababu asipofanya hivyo analinda udhaifu katika nchi. 

No comments: