Saturday, January 5, 2013

MVUA YAHARIBU RELI, SAFARI MWANZA-KIGOMA ZAFUTWA...

Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi, imeharibu tuta la reli katika eneo la Mikese, mkoani Morogoro na kuulazimu uongozi wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), kuahirisha safari ya treni ya Bara iliyokuwa ifanyike jana mchana.
Kuahirishwa kwa safari hizo kwenda katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Kigoma na Mwanza kulithibitishwa jana na Meneja Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez.
Kupitia taarifa yake iliyoitoa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mhandisi Kipallo Kisamfu, Maez alisema: Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania – TRL, unawataarifu abiria wote na wananchi kwa jumla kuwa kutokana na kuharibika njia ya reli eneo la Stesheni ya Mikese jana usiku, safari ya treni ya abiria ya kutoka Dar es Salaam kwenda Bara iliyopangwa kuondoka leo Ijumaa (jana)  Januari 04, 2013 saa 8:30 mchana  haitakuwepo.
“Taarifa ya siku ya kuondoka itatangazwa baadae kulingana na ushauri wa Jopo la Wataalamu wa TRL waliopelekwa kusimamia ukarabati wa eneo hilo.  Uongozi wa TRL unaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.”
Hata hivyo, taarifa zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinasema kuwa, juhudi za wataalamu kukarabati eneo lililoharibika zimetoa matumaini ya kurejea kwa usafiri wa treni na kwamba huenda ukarejea leo huku safari iliyoahirishwa ikitarajiwa kuwa saa 11 jioni.

No comments: