Wednesday, January 2, 2013

DEREVA WA MWALIMU NYERERE AFARIKI DUNIA...

Mwalimu Nyerere.

Aliyekuwa dereva wa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, amefariki dunia.
Mzee Iddi Juma Simba (97) alifariki dunia jana alfajiri baada ya kuugua kwa muda mfupi, imeelezwa.
Akitoa taarifa za kifo cha Mzee Simba jana, shemeji yake Kibwana Kilagi, alisema mauti yalimkuta Mzee Simba nyumbani kwake mtaa wa Mtoni mjini hapa na kwamba maziko yalitarajiwa  kufanyika jana alasiri katika makaburi ya familia yaliyoko karibu na Chuo cha Kilimo (SUA) mjini hapa.
 “Mzee Simba,  mimi  ni shemeji yangu. Ameniolea dada yangu, na tangu alipoanza kuugua kwa kupooza upande mmoja, nilikuwa hapa kumuuguza hadi leo saa 9:00 alfajiri alipotutoka,” alisema Kilagi.
Baadhi ya wananchi waliofika nyumbani kwa marehemu wakiwamo waumini wa dini ya Kiislamu, walimtaja kuwa muumini mzuri wa dini hiyo asiyependa dhuluma kwa watu wengine.
Katibu wa Kamati ya Kufuatilia Mali za Waislamu Morogoro, Mussa Kimoje, alisema Mzee Simba wakati wa uhai wake alikuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo tangu mwaka 2004 .
Akihojiwa na mwandishi wa habari hizi wakati wa uhai wake kwa ajili ya maandalizi ya makala za Miaka 50 ya Uhuru mwaka juzi, Mzee Simba alipata kueleza jinsi alivyoahidiwa fedha  na Waingereza ili atekeleze njama ya  kumuua  Mwalimu Nyerere wakati akimwendesha akakataa kutekeleza njama hizo.

No comments: