Wednesday, January 2, 2013

BEI YA PETROLI YASHUKA, SASA SHILINGI 1,993 KWA LITA...


Watumiaji wa mafuta jamii ya petroli wameanza mwaka mpya wa 2013 kwa unafuu, kutokana na bei ya nishati hiyo kushuka kwa mwezi huu.
Kuanzia leo bei ya rejareja ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua, ambapo petroli imepungua kwa Sh 126 kwa lita sawa na asilimia 5.96; dizeli kwa Sh 32 sawa na asilimia 1.60 huku mafuta ya taa yakishuka kwa Sh 50.74 sawa na asilimia 2.50.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)  kwa mkoani Dar es Salaam petroli ni Sh 1,993, dizeli Sh 1,967 na mafuta ya taa Sh 1,973 kwa lita, wakati kwa Arusha, petroli inauzwa Sh 2,077, dizeli Sh 2,051 na mafuta ya taa Sh 2,057.
Kwa bei hiyo, mkoani Dodoma petroli inauzwa Sh 2,051, dizeli Sh 2,026 na mafuta ya taa Sh 2,031 kwa lita; huku Iringa, nishati hiyo ikiuzwa Sh 2,057 (petroli), Sh 2,057 (dizeli) na Sh 2,037 (mafuta ya taa). Mkoani Njombe, petroli inauzwa Sh 2,085, dizeli Sh 2,059 na mafuta ya taa Sh 2,065 kwa lita.
Mkoani Kagera, wilayani Bukoba petroli inauzwa Sh 2,208, dizeli Sh 2,182 na mafuta ya taa Sh 2,188; nako Geita petroli inauzwa Sh 2,158, Sh 2,132 kwa dizeli na Sh 2,138 kwa mafuta ya taa. Petroli mkoani Kigoma inauzwa Sh 2,223, dizeli Sh 2,198 na mafuta ya taa Sh 2,203.
Kwa mujibu wa Ewura, bei kikomo ya jumla ya nishati hiyo mkoani Dar es Salaam ni Sh 1,918.60 kwa petroli, Sh 1,892.97 kwa dizeli na Sh 1,898.62 kwa mafuta ya taa.

No comments: