AFYA YA MKURUGENZI UPELELEZI MAKOSA YA JINAI BADO TETE...

Advera Senso.
Afya ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba imezidi kuwa tete katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam anakopatiwa matibabu ingawa kuna taarifa kuwa anaendelea vizuri.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alisema jana kuwa leo Jeshi hilo litatoa taarifa kamili ya kinachomsibu Kamanda huyo na hali yake kwa ujumla inavyoendelea.
“Leo (Jana) kwa kweli anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku nyingine na yupo chini ya uangalizi wa madaktari,” alisema Senso katika viwanja vya hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk Jaffer Dharese,  taarifa za kupelekwa nje ya nchi pamoja na matatizo yanayomsumbua zitatolewa leo.
“Tumeshauri Manumba apelekwe nje ya nchi na ndio maana tutawaeleza kila kitu kesho (leo) kuhusu hali hiyo,” alisema.
Dharese alisema Kamanda huyo ameweka historia ya wananchi wengi kufika hospitalini hapo kumjulia hali.
Wakati hayo yakiendelea, mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa siyo msemaji, alisema wazo la kumpeleka Manumba nje ya nchi linaweza kuwa gumu kutokana na hali yake ilivyo.
“Huyu anapumulia mashine, kumsafirisha akiwa katika hali hii ni jambo gumu kidogo, sijui itawezekanaje,” alisema.
Hata hivyo mmoja wa ndugu wa Manumba alimdokeza mwandishi kuwa angalau hivi sasa mgonjwa huyo ameanza kurejewa na fahamu.
“Yaani sasa hivi tunaona angalau ana unafuu kwani ukimgusa unaona anashtuka kuonyesha anahisi kitu tofauti na ilivyokuwa huko nyuma,” alisema.

No comments: