MAKAMU WA RAIS ATAKA WANAZUONI KUTAFAKARI VURUGU ZA KIDINI...

Dk Mohammed Gharib Bilal.
Makamu wa Rais,  Dk Mohammed Gharib Bilal amewataka   wanazuoni wa Bara la Afrika,  kutafakari matukio mbalimbali ya vurugu za kidini yaliyotokea hapa nchini hivi karibuni.
Amewataka watafakari hilo kwa lengo la kuweka mustakabali mzuri wa kuishi kwa kuheshimiana baina ya wafuasi wa dini kuu mbili za Kiislamu na Kikristo.
Dk Bilal alisema hayo jana katika ufunguzi wa mkutano wa pili wa wanazuoni hao, unaofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
“Imani si ugomvi bali imani, inapaswa itujenge kimaadili na moja katika tunu za maadili ni kuishi vizuri na watu wengine hata kama si wa imani yako,” alibainisha.
Alihimiza umuhimu wa kujenga maelewano mazuri baina ya wafuasi wa dini mbalimbali. Alionya kuwa vinginevyo Bara la Afrika linaweza kushuhudia migogoro mingi ya kidini, kama ilivyoanza kujitokeza  Nigeria na hata hapa nchini. 
Alisema Bara la Afrika lina waumini wengi wa dini mbalimbali,  zikiwemo za Kiislamu na Kikristo. Alisisitiza kuwa bila uwepo wa maelewano mazuri baina ya wafuasi wa dini hizo, suala la mifarakano ni lazima litatokea.
Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa elimu ya mwongozo na ile ya maarifa ya dunia kwa Waislamu na kusema itawawezesha kutatua matatizo yanayowakabili wananchi, yakiwemo ya uharibifu wa maadili, uasherati, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, ukosefu wa ajira na unyanyasaji wa kijinsia.
Alitoa changamoto kwa wanazuoni wa Kiislamu na viongozi wengine wa dini,  kuangalia ni jinsi gani utandawazi hautoathiri imani na maadili ya waumini, lakini pia ni jinsi gani waumini watanufaika na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, yaliyofikiwa na mwanadamu hivi sasa.
Malengo ya Umoja huo wa Wanazuoni Barani Afrika ni pamoja na kutilia nguvu masuala ya elimu, ushirikiano na kuheshimiana baina ya jamii mbalimbali barani Afrika.
Makamu wa Rais alisema malengo hayo ni mazuri na ya kujenga,  ambayo kama yakiwekwa katika matendo, itaondoa ile picha hasi kuwa Waislamu ni watu wenye kufarakana, wasio na elimu, wasioheshimu dini za wengine na wasiotambua nafasi na mchango wao katika maendeleo ya nchi hizo.
Awali,  Rais wa Jumuiya ya Wanazuoni Tanzania,  Sheikh Suleiman Kilemile alisema kufanyika kwa mkutano huo wa wanazuoni hapa Tanzania ni heshima kwa Taifa, kwa kuwa huo ni mkutano wa pili tangu umoja huo uanzishwe.
Alisema mkutano huo wa siku tatu, umekusudia kuzungumzia masuala mbalimbali yatakayojenga misingi ya dini hiyo ndani na nje ya Bara la Afrika.
Alisema mkutano huo unahudhuriwa na wanazuoni na walinganiaji wa Kiislamu kutoka nchi takribani 24 zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara na nje ya Bara la Afrika.

No comments: