MWAKYEMBE ATUPILIA MBALI WAZO KA KUKODI INJINI ZA TRENI...

Dk Harrison Mwakyembe.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, amelazimika kukataa kuingia mkataba wa kukodisha injini za treni kutoka Afrika Kusini, baada ya kulazimishwa kukodi injini 18 kwa miaka nane.  Injini hizo zinatafutwa ili kufufua usafiri wa reli nchini.
Dk Mwakyembe alisema hayo juzi jijini Mwanza katika mazungumzo ya muda mfupi na gazeti hili.  Alisema hayo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa ziara ya siku moja jijini Mwanza.
Alisema  wakati Wizara ilipoanza kutafuta namna ya kufufua usafiri wa reli, walituma wataalamu kwenda Afrika Kusini kukodisha injini na ilikuwa imetenga Sh bilioni 40 kwa ajili ya ukodishaji huo.
“Kule tulikuta gharama ni kubwa, kuliko ambavyo tungewatumia wataalamu wetu wenyewe, maana tuliambiwa gharama ya kukodi injini moja ya treni kwa siku ni Sh milioni 3. Tena kampuni tuliyoomba itukodishie kwa miaka miwili, ikakataa, ikataka lazima itukodishie kwa miaka 8 na
tulitakiwa tukodishe injini 18 za treni, tukaona haitawezekana,” alifafanua.
Alisema baada ya kuona gharama hizo, alikwenda kuzungumza na wahandisi na mafundi wa Shirika la Reli, ambao walimhakikishia kuwa wanao uwezo wa kutengeneza injini zilizokufa wao wenyewe.
“Sasa utashangaa, wahandisi na mafundi wetu wa ndani, wameweza kukarabati injini kwa shilingi milioni 900 inayodumu kwa miaka 8 tena bila ya kukarabatiwa,” alisema.
Akizungumzia usafiri wa reli kwa Kanda ya Ziwa, Dk Mwakyembe alisema kuwa Wizara yake inatarajia kuongeza safari za kutoka Dar es Salaam - Mwanza kutoka mara mbili kwa wiki hadi mara tano.
Alisema wapo watu wanaodhani kuwa huduma ya usafiri wa treni, iliyoanzishwa hivi karibuni haitadumu muda mrefu, lakini, kusema ukweli huduma hiyo itaendelea. Alisisitiza kuwa azma ya Serikali ni  kuimarisha huduma ya usafiri wa reli kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa. 
Aliwataka wakazi wa mikoa hiyo kuendelea kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kuimarisha huduma hiyo, ikiwa ni pamoja na kujipanga kukabiliana na changamoto za muda mrefu zilizokuwepo ndani ya Shirika la Reli.
“Niwajulishe wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, nia yetu ni kuhakikisha kuwa wanapata huduma hii ya usafiri wa reli mara tano kwa wiki,” alisema.

No comments: