Saturday, December 8, 2012

KIAMA KWA WACHIMBAJI WADOGO SASA CHAWADIA...

Mmoja wa wachimbaji wadogo akiwa amejipumzisha baada ya kazi ngumu.
Serikali imetangaza kiama kwa wachimbaji wadogo waliohodhi maeneo makubwa bila kuyaendeleza na kusema itawanyang’anya maeneo hayo na kuwapatia wengine.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akizungumza na viongozi wa wachimbaji wadogo katika Mkutano wa mwaka unaofanyika katika ukumbi wa zamani wa Bunge wa Pius Msekwa.
Pamoja na kutoa kauli hiyo alisema serikali imetenga Sh bilioni 8.9 kwa ajili ya kuboresha mazingira kwa wachimbaji wadogo na inakusudia fedha hizo zilete tija katika uchumi wa mtu binafsi na taifa.
Waziri huyo alisema wazi kwamba suala la uchimbaji wa madini ni suala la kiuchumi na hodhi iliyofanyika ndiyo inawafanya watu wadhani kodi ni kubwa na kuanza kuchanganya masuala ya kiuchumi na kisiasa.
Aliwaambia wachimbaji wadogo kuwa uchimbaji wa madini ni suala la kiuchumi na kutaka yasiingizwe kwenye uchimbaji, hali inayozuia sekta hiyo kukua inavyostahili ili kuchangia ajira na uchumi.
“Kuna watu ambao si wachimbaji wadogo, mtu mwenye viwanja 100 si mchimbaji mdogo, ndiyo maana watu wanalia kodi ni kubwa; mtu  mwenye viwanja 500 inakuwa ni vilio, ameshikilia viwanja vingi  anasema kodi juu akitokea mtu anamuuzia, hao ndiyo wamekuwa wakileta kelele za kupunguziwa kodi, jambo kama hili sitaki kulisikia tena.”
Alisema, “katika kushughulikia suala hili sheria za kuwanyang’anya wasioendeleza viwanja itafanya kazi; na kama mchimbaji una mashimo mawili utalipa kodi kwani hakuna faida ya kuwa na maeneo makubwa bila kuwa na uzalishaji na kodi hulipi.
“Hata kampuni kubwa tumezinyang’anya  maeneo na wengine wanatoa wenyewe afadhali kuwa na wachimbaji wachache wanaochimba kwa teknolojia ya kisasa na si kuwa na  utitiri wa wachimbaji bila kuwa na mavuno,” alisema.
Alisema kuwa, uchumi wa karne ya 21 ni sawasawa na sayansi ukijumlisha teknolojia na ubunifu ni lazima kuwe na faida kubwa kwa mhusika na uchumi wa taifa.
Alisema hali hiyo inaweza kubadilika kama mtu ataacha kuhodhi viwanja na kuchimba anapoweza na hivyo kuzalisha kwa mujibu wa uwezo wake na kuwaachia wengine nao wachimbe kwa uwezo wao, na katika hilo hakuna siasa.
“Hapo hakuna neno  siasa, malumbano, visingizio; ukiangalia sisi wachimbaji wadogo,  humo hatumo kabisa, ina maana Serikali imeazimia kubadili mfumo wa kufanya kazi na sisi wachimbaji wadogo ndiko tunakokwenda” alisema
“Wachimbaji wadogo msichanganye uchimbaji  na siasa mwaka wa kugombea Udiwani Ubunge na Urais, tunapoelekea mwaka 2015  tuongelee uchumi na maendeleo na si siasa na vyeo,” alisema.

No comments: