Wednesday, December 12, 2012

ASKARI MAGEREZA AUAWA AKIDHANIWA MWIZI...

Mwili wa Ezekiah Gambi.
Mwili wa Abel Mwakajinga.

Askari Magereza, Abel Mwakajinga (24), ameuawa kwa kupigwa na kuchomwa moto na wananchi baada ya kupigiwa kelele za mwizi, aliyekuwa akijaribu kupora pikipiki.
Mwakajinga aliyekuwa likizo, aliuawa Jumamosi iliyopita katika Kijiji cha Ukwile saa 10:00 jioni pamoja na ndugu yake, Ezekiah Gambi (30), alipokuwa akijaribu kumkamata mtuhumiwa wa mauaji ya ndugu yake, Laiton Nganya.
Akisimulia kisa hicho, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ukwile, Osiah Mtawa alisema kabla ya mauaji hayo, Mwakajinga na Ezekiah walikuwa wakimtuhumu Nganya kwa kumuua ndugu yao, Salum Gambi aliyeuawa Novemba 14, mwaka huu.
Mtawa alidai kutokana na tuhuma hizo, siku ya tukio askari Mwakajinga na ndugu yake Ezekiah walipata taarifa ya kuonekana kwa Nganya katika kijiji hicho, hivyo waliamua kwenda kumkamata.
Kwa mujibu wa madai ya Mtawa, askari Mwakajinga na Ezekiah walikodi pikipiki kutoka Kijiji cha Mlowo kwenda kijijini hapo kumkamata Nganya.
Mtawa alidai kuwa dereva wa bodaboda waliyemkodi, Zemu Kayila, alikuwa akiwasiliana na mtuhumiwa waliyekuwa wakimfuata, akimpa taarifa za safari hiyo. 
Baada ya kufika katika kijiji hicho, Mtawa alidai Mwakajinga alishuka na kwenda moja kwa moja kumkamata mtuhumiwa, lakini kabla ya kutimiza malengo yake, mtuhumiwa aliyekuwa amejipanga, alipiga yowe la kuomba msaada kwa wanakijiji, akisema amevamiwa na wezi wa pikipiki.
Mwenyekiti huyo wa kijiji alidai kutokana na mayowe hayo, wakazi wa kijiji hicho walijitokeza na kuanza kuwashambulia kwa kuwapiga kwa kutumia vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili ya askari huyo na mwenzake na kuwachoma moto na  kusababisha vifo vyao.
“Niliamua kutoa taarifa mara moja Polisi ambapo  ilipofika saa 12:00 jioni, askari polisi wakaja kuwachukua marehemu wote wawili, yaani askari magereza na ndugu yake na kuwapeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi katika Mji Mdogo wa Vwawa kwa ajili ya uchunguzi,” alidai.
Mdogo wa Ezekiah, aliyejitambulisha kwa jina la Godfrey Gambi (26), alisema ndugu zake walikwenda katika kijiji hicho kumkamata mtuhumiwa wa mauji ya ndugu yao, ambaye aliuawa kwa kupigwa na vitu vyenye ncha kali katika Kijiji cha Chizumbi mpakani mwa wilaya ya Ileje na Mbozi, kabla ya mtuhumiwa huyo kukimbilia kusikojulikana.
“Baada ya kuona mtuhumiwa hajakamatwa tulifanya uchunguzi kama wanandugu na kubaini kuwa mtuhumiwa huyo yupo katika Kijiji cha Ukwile, ndipo hawa ndugu wakachukua uamuzi wa kumfuata kumkamata,” alisema Gambi.
Alisema miili ya ndugu zake ilifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na kukabidhiwa kwa familia na kuzikwa Jumapili iliyopita, ambapo askari magereza alizikwa katika Kijiji cha Mbebe wilayani Ileje.
Akizungumza kwa njia ya simu ya kiganjani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alikiri kuwa na taarifa za tukio hilo na na kusema tayari watuhumiwa wa mauaji hayo, wametambuliwa na utaratibu unafanyika ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

No comments: