Wednesday, November 21, 2012

WATAKA SARE ZA VYAMA VYA SIASA ZIPIGWE MARUFUKU...

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa maoni, wamependekeza sare za vyama vya siasa zipigwe marufuku kwenye Katiba mpya kwa maelezo kuwa zinachochea mgawanyiko kwa Watanzania.
Wenye hoja hiyo pia walitaka vyama vya siasa viruhusiwe kuendesha shughuli zao kwa kutumia Bendera ya Taifa badala ya kupeperusha bendera za vyama vyao ambazo zinaonesha mgawanyiko wa kiitikadi.
Hayo ni miongoni mwa maoni yaliyotolewa jana katika Viwanja vya Miburani, Temeke ambako Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikuwa ikikusanya maoni.
Kundi hilo la wajumbe wa Tume liko chini ya Salama Kombo Ahamed ambaye ni Kaimu Mwenyekiti, Dk Salim Ahmed Salim na Profesa Palamagamba Kabudi.
Wananchi katika eneo hilo, walitaka Katiba mpya iweke idadi ya vyama vya siasa vinavyoruhusiwa nchini, ili  kuwe na vyama vichache vyenye nguvu kuliko utitiri wa vyama uliopo sasa.
"Hizi sare za vyama vya siasa zimeongeza chuki miongoni mwetu na kusakamana kuwa yule wa CCM yule wa Chadema, ni vyema vipigwe marufuku kulinda umoja wetu," alisema Kapuru Kapama.
Kapama alisema nchi ambazo hazitumii sare wala bendera za kisiasa hata uchaguzi unapokwisha, wananchi hubaki wamoja kwani wote hugombania nchi yao kuliko nchi ambazo zinapeperusha bendera   na kuvaa sare za vyama.
Esther Mwakitalima alitaka idadi ya vyama vya siasa ipungue lakini pia akataka askari Polisi na wa majeshi yote wasipige kura kwani ndio wamekuwa chanzo cha matatizo katika uchaguzi mbalimbali.
"Hawa siku ya uchaguzi wawe walinzi tu, waachane na kupiga kura, wamekuwa chanzo cha matatizo katika uchaguzi nchini," alisema Mwakitalima.
 Melikioi Ngonyani alitaka ardhi iendelee kumilikiwa na Serikali lakini akataka ardhi ambayo chini yake kuna rasilimali kama madini, mafuta na gesi, mwekezaji anayetaka kuwekeza kwenye maeneo hayo alipe asilimia 30 kama mrabaha.
"Hili la wawekezaji kuja wanatulipa asilimia 3 au 5 ni unyonyaji mkubwa, na kwa kuwa hatuna uwezo wa kuingia mikataba ni vema Katiba iainishe kuwa mwekezaji aje lakini alipe mrabaha asilimia 30, na kama hataki aondoke," alisema.
James Matita alitaka Katiba mpya ikataze ubaguzi katika ajira, akidai kuwa kwa sasa watoto wa vigogo wanapendelewa katika ajira kwenye taasisi nzuri kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT). 
Twaiba Mtumbuka alipinga sheria ya ugaidi kuwa inaonea Waislamu, hivyo akapendekeza ifutwe. "Maana mtu akifuga ndevu tu anaitwa gaidi, wakati ni suna ya Mtume Muhammad (S A W)."
Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Ahmed Mohamed ambaye alisema sheria hiyo ya ugaidi ni kandamizi kwani mtu akituhumiwa tu, anaweza kuuawa na vyombo vya Dola.
"Sisi hii sheria inatunyanyasa Waislamu," alisema Mohamed ambaye kwenye maoni yake pia alitaka kinga ya kumshitaki Rais iondolewe mara amalizapo madaraka na uteuzi wa viongozi uzingatie uwiano wa dini.
Shida Salute ambaye ni mwalimu, alipinga mfumo wa wanafunzi wa darasa la saba kufanyiwa mtihani wa maswali ya kuchagua, kuwa imekuwa chanzo cha wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kufaulu.
"Mwanafunzi mbumbumbu anafanya ‘ana ana anado’ na anapatia jibu, akienda sekondari hajui kusoma, ni vyema utaratibu wa awali wa wanafunzi kujieleza uendelee," alisema Salute.

No comments: