Wednesday, November 21, 2012

MWALIMU BORA KUJIZOLEA SHILINGI MILIONI 40 TASLIMU...

Bodi ya Tuzo za Walimu Bora Tanzania, imetangaza zawadi za washindi wa tuzo hizo, ambapo mshindi wa kwanza atajinyakulia Sh milioni 40.
Mbali na fedha, mshindi huyo pia atapewa ufadhili wa kusoma kwa miaka mitatu ambapo kila mwaka atapewa Sh milioni tano.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Emmanuel Mjema, alisema washindi hao watagawanywa katika makundi mawili na kuzawadiwa, lengo likiwa ni kurudisha hadhi ya walimu.
Alisema mshindi wa pili katika tuzo hizo, atapata Sh milioni 30 pamoja na ufadhili wa kusoma miaka mitatu na kila mwaka atapewa Sh milioni nne.
Profesa Mjema alisema mshindi wa tatu atapewa Sh milioni 20 pamoja na Sh milioni tisa kwa ajili ya kusoma kwa miaka mitatu.
Mshindi wa nne atazawadiwa Sh milioni 10, pamoja na ufadhili wa kusoma Sh milioni 6 huku mshindi wa tano akizawadiwa Sh milioni tano na ufadhili wa kusoma wa Sh milioni 6.
Wa sita hadi wa 10 watapata pikipiki moja moja zenye thamani ya Sh milioni mbili na laptop yenye thamani ya Sh milioni 1.5.  
Profesa Mjema alisema kwa upande wa washindi wa masomo sita yanayoshindanishwa, kila somo watapatikana washindi 10 wa shule za msingi na 10 wengine wa sekondari ambapo jumla ni washindi 120 na kila mmoja atazawadiwa Sh 300,000 na baiskeli yenye thamani ya Sh 200,000 kila mshindi.
Alisema tuzo hizo zimelenga walimu wote wa shule za msingi na sekondari ambazo ni binafsi na za serikali lengo likiwa ni kuonesha usawa na thamani kwao katika kukuza maendeleo ya nchi. Masomo yatakayoshindaniwa ni Sayansi, Hisabati, Kiswahili, Jiografia, Historia na Kiingereza.
Alisema fomu za ushiriki zitaanza kupatikana rasmi Desemba 15 hadi Februari 10 mwakani katika matawi yote ya Benki ya Posta Tanzania katika mikoa yote Bara.
Profesa Mjema alitaja vigezo 21 vya washiriki wa tuzo hizo  vilivyowekwa kwa kila mshiriki akisema ili mwalimu ashiriki lazima awe raia wa Tanzania, umri wa kati ya miaka 18-54, awe na cheti cha kuzaliwa au cha darasa la saba au kitambulisho cha kupigia kura au pasipoti.
Pia mshiriki ni lazima awe ameajiriwa ualimu kwa kipindi cha miaka mitano na kuendelea, awe na mahudhurio mazuri kazini na kuhudhuria vipindi vyote vya kufundisha darasani, awe mtu wa kujitolea kwa maendeleo ya elimu nchini na awe mwadilifu kazini na katika jamii anamoishi.
Aidha, anatakiwa awe anajua wajibu wa kutimiza malengo ya kazi yake kwa kuandaa maazimio ya kazi, mandalizi ya somo, awe na haiba inayojitosheleza na ushirikiano mzuri na walimu wenzake na wanafunzi.
“Mshiriki pia anatakiwa awe mbunifu na anayemudu kukabiliana na changamoto zilizopo yakiwamo mazingira duni ya kazi yake, asiwe na tuhuma za rushwa au aliyepata kuwa na kosa la jinai, awe anavaa uasilia kwa vitendo na awe na matokeo mazuri kwa wanafunzi kwa ngazi zote anazofundisha,” alisema.
Alisema pia mshiriki anatakiwa awe mwajiriwa serikalini au sekta binafsi, awe tayari kushiriki mambo ya jamii ikiwamo michezo, mazingira na majanga, awe anaendana na sera ya elimu, awe anayekubalika na wafanyakazi wenziwe na hata wanafunzi kwa jumla.
Mshiriki wa tuzo hizo pia anatakiwa asiwe ameacha kazi ya ualimu na kuirudia na awe amesomea taaluma ya ualimu katika chuo au vyuo vinavyotambulika kiserikali.

No comments: