Wednesday, November 21, 2012

TAARIFA KAMILI HUKUMU YA KIFO YA WANAJESHI WATATU...

Wanajeshi waliomuua mtoto wa Chifu Fundikira wakiwa mahakamani jana. Kutoka kulia ni Sajini Rhoda Robert, Koplo Ally Ngumbe na Koplo Mohamed Rashid.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu kunyongwa hadi kufa wanajeshi watatu baada ya kuwakuta na hatia ya kumuua kwa kukusudia Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa marehemu Chifu Abdallah Fundikira.
Washitakiwa hao ni Sajini Rhoda Robert (42) wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha Mbweni, Koplo Ally Ngumbe (37) wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Kunduchi na Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni. 
Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Zainabu Mruke alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka katika kesi hiyo umethibitisha kuwa washitakiwa waliua kwa kukusudia.
Alisema pamoja na kuwa hakuna shahidi aliyeshuhudia washitakiwa wakimuua Swetu, lakini ushahidi wa mazingira ambao haujaacha shaka, umeunda muunganiko wa ushahidi uliothibitisha washitakiwa kutenda kosa hilo.
Jaji Zainab alisema upande wa mashitaka ulithibitisha kuwa Swetu aliuawa kutokana na majeraha yaliyotokana na kupigwa na kitu kichwani na ushahidi wa daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na ripoti ya uchunguzi, vilithibitisha hilo.
Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa mahakamani hapo kama kielelezo, kifo cha Swetu kilitokana na kukandamizwa na kitu kisicho na ncha kali, jambo lililosababisha damu kuvuja kichwani na pia alikutwa na majeraha mengi ya aina moja.
Alisema Januari 23 mwaka juzi, Swetu akiwa na dereva teksi katika makutano ya barabara za Kawawa na Mwinjuma, walikwaruzana na wanajeshi hao ndipo wakampiga na watu walipofika, walidai kuwa Swetu alitaka kuwapora gari na kudai wanampeleka Kituo cha Polisi Oysterbay.
Hata hivyo, hawakufanya hivyo na baadaye walikutwa eneo la Msikiti wa Jamatini huku mwili wa marehemu ukiwa umelala kifudifudi bila nguo zaidi ya soksi mguu wa kulia ambapo katika utetezi wao walidai kuwa Swetu alivua nguo na kujirusha kwa kuwa hakutaka kupelekwa Polisi.
Alisema kwa sababu washitakiwa walikuwa watu wa mwisho kuonekana na marehemu, walitakiwa kutoa maelezo ya kina na yasiyoacha shaka ya nini kilichomkuta Swetu, lakini maelezo yao yalizua utata kwa sababu walikiri kupigana na Swetu na kukutwa naye akiwa hajitambui tena bila nguo.
Jaji Zainab alisema washitakiwa walidai wanampeleka Swetu Kituo cha Polisi Oysterbay, lakini hawakufanya hivyo na badala yake walipita vituo viwili vya Polisi wakidai wanajua Kituo cha Kati pekee wakati wameishi Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20, pia marehemu alitoka eneo la tukio akiwa na nguvu.
Aliongeza kuwa maelezo ya washitakiwa kuwa alivua nguo na kujirusha hayakuwa na ukweli, kwa kuwa askari watatu wasingeweza kumwacha mtuhumiwa afanye hivyo, wakati wakimpeleka kituoni na ripoti ya daktari haijaonesha kama alikuwa na mpasuko kichwani.
Jaji Zainab alisema washitakiwa walimuua kwa kukusudia, kwa sababu walikuwa na nia ovu ambapo kabla na hata baada ya tukio, Sajini Rhoda alitoa maneno ya vitisho, pia walimpiga kichwani na kumvua nguo zote.
Ingawa hakuna aliyeshuhudia washitakiwa wakimuua Swetu, lakini Jaji Zainab alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka na washitakiwa walishindwa kutoa maelezo ya kina kuhusu kifo cha Swetu.
Baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, ndugu wa marehemu Swetu waliangua kilio mahakamani na wengine kuzimia ambapo dada yake, Rehema Fundikira alisema anaishukuru Mahakama kwa kuwa imetenda haki.
“Tunalia si kwa furaha bali kwa uchungu, ni kama msiba umerudi kwa sababu imenimekumbusha siku mdogo wangu alivyouawa kinyama, lakini namshukuru Mungu haki imetendeka,” alisema Rehema.
Wakili wa washitakiwa Luge Kaloli alidai hawajaridhika na hukumu hiyo na wanatarajia kukata rufaa.

No comments: