Thursday, November 22, 2012

WANAJESHI 10 WADAIWA KUFANYA MAUAJI KWENYE BAA MBEYA...

Kamanda Diwani Athuman.
Wakati habari za kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa wanajeshi watatu zikiwa bado mbichi, watu 14 wakiwamo askari 10 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa kikosi cha 44KJ Kambi ya Mbalizi wilayani hapa, wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman alisema jana kuwa askari hao wanatuhumiwa kumwua Petro Sanga (25)  Novemba 18 katika baa ya Power Pub.
Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, siku hiyo saa 3 usiku  baa hiyo ilivamiwa na kundi la watu waliodaiwa kuwa askari wa JWTZ na kushambulia wateja akiwamo Sanga.
Juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwahukumu kunyongwa hadi kufa wanajeshi watatu baada ya kuwakuta na hatia ya kumuua kwa kukusudia Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa marehemu Chifu Abdallah Fundikira.
Wahukumiwa hao ni Sajini Rhoda Robert (42) wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha Mbweni, Koplo Ally Ngumbe (37) wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Kunduchi na Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni. 
Wakati wa shambulizi hilo la baa, Sanga alichomwa kisu shingoni na midomoni na alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Teule ya Ifisi. Wateja wengine sita pia walijeruhiwa kwa kipigo hicho.
Akisimulia, Kamanda Athumani alisema  askari hao walikuwa wakilipiza kisasi baada ya walinzi wa baa hiyo kumpiga askari mwenzao, Geodfery Matete (30) Novemba 17, alipokuwa katika kilabu cha pombe za kienyeji cha DDC.
“Wakati Sanga na wateja wengine wakiendelea kuburudika kwa vinywaji, watuhumiwa walivamia na   kuwashambulia huku Sanga akipigwa mateke, mikanda, marungu, sime na mapanga na kuchomwa kisu wakati akijaribu kujiokoa kwa kukimbilia baa nyingine ya Vavenemwe.
“Kutokana na majeraha ya kisu, Sanga alipoteza fahamu ndipo wasamaria wema wakamkimbiza katika hospitalini katika mji mdogo wa Mbalizi. Huko alifariki dunia akitibiwa baada ya kuvuja damu nyingi,” alisema Kamanda Athumani.
Kamanda alisema pia Polisi inashikilia walinzi wanne, Frenk Mtasimwa (25), Mure Julius (26), Omari Charles (28) na Reginald Mwampete wakazi wa Izumbwe, Mbeya kwa tuhuma za kumshambulia askari wa JWTZ.  
Hata hivyo, alikataa kutaja majina ya wanajeshi wanaoshikiliwa kwa mauaji kwa madai kuwa atawataja baadaye, kwa kuwa bado uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Kuhusu tukio la wanajeshi watatu kuhukumiwa kifo, ilidaiwa mapema mahakamani kuwa  Januari 23 mwaka juzi, Swetu akiwa na dereva teksi katika makutano ya barabara za Kawawa na Mwinjuma, walikwaruzana na wanajeshi hao ndipo wakampiga.

No comments: