Thursday, November 22, 2012

AJALI YA BASI LA NGW'ALU EXPRESS YAUA WATU MWANZA...

Ernest Mangu.
Watu watatu wamefariki dunia na wengine 24 kujeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha basi mali ya Ng’walu Express ya mkoani Mwanza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Ernest Mangu alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea saa 12.30 asubuhi katika eneo la Isangijo wilayani Magu wakati basi hilo lilipokuwa likitoka jijini Mwanza kwenda Musoma mkoani Mara.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni basi hilo lilipofika eneo hilo, dereva alishindwa kulimudu kutokana na mwendokasi lililokuwa nao, hali iliyolifanya kutoka nje ya barabara na kusababisha vifo vya watu watatu.
“Inaonekana dereva alishindwa kulimudu gari hali iliyosababisha kutoka nje ya barabara na kusababisha ajali, ambapo watu watatu ambao majina yao hayajafahamika walifariki palepale na wengine 24 kujeruhiwa,” alisema Kamanda Mangu.
Kamanda Mangu alisema maiti za watu waliokufa wamehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, ilihali majeruhi wakitibiwa katika Hospitali ya Bugando na ile ya Mkoa ya Sekou Toure.
Katika tukio lingine, Kamanda Mangu alisema Levina Chande (60) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Barabara ya Kenyata jijini Mwanza, alikutwa ndani akiwa amekufa huku mwili wake ukionesha kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Alisema mauaji hayo inaonekana yalitokea Novemba 17, mwaka huu saa 2.00 asubuhi baada ya Polisi kujulishwa na majirani kuwa nyumba ya marehemu ilikuwa imefungwa kwa siku nzima bila ya kufunguliwa, hali iliyowapa wasiwasi.
Aidha, katika tukio la tatu, Kamanda Mangu alisema mtu mmoja mwanamume mwenye umri kati ya miaka 35-45 katika Mtaa wa Nyanguli, Kata ya Ilemela alikutwa amekufa maji katika Ziwa Victoria.
Kamanda Mangu alisema mwili wa mtu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure ukisubiri ndugu kwa ajili ya kutambuliwa ili usafirishwe kwao.

No comments: