Thursday, November 22, 2012

ASKOFU MOKIWA AFICHUA KUWA UKIMWI SASA NI BIASHARA...

Askofu Dk Valentino Mokiwa.
Rais wa Baraza la Makanisa Afrika ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa, ameshutumu viwanda vya dawa baridi duniani kwa kugeuza Ukimwi biashara.
Akizungumza katika ufunguzi wa semina ya wachungaji wa makanisa yanayounda Jumuiya ya Makanisa nchini jana Dar es Salaam, Dk Mokiwa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa Jumuiya hiyo, alisema Ukimwi unaendelea kutesa watu kwa sababu viwanda vya dawa vinataka viendelee kuuza daswa za kupunguza makali (ARVs). 
Alisema, anaamini dawa ya ugonjwa huo ipo, kwa sababu watengenezaji ambao ni viwanda vya dawa baridi duniani, walikwishafanikiwa kuzalisha za kupunguza makali, hivyo isingekuwa vigumu kutengeneza za kutibu.
“Hili ni jambo linaloniuma sana, kwa sababu watengeneza dawa za binadamu wanaulea Ukimwi kwa makusudi ili wajinufaishe kifedha. Nafahamu wanauelewa ukweli kuhusu jambo hili, lakini wanaendelea kuishikilia siri kuhusu dawa zinazotibu ili wauze ARVs. 
“Ukimwi umegeuzwa mradi wa kujipatia fedha na umekuwa kweli mradi wa fedha kwa kuwa hata magari sasa yanaugua huu ugonjwa. Kila unapopita unaona yamebandikwa mabango au kuandikwa ‘ugonjwa wa Ukimwi’. Watu wanautumia kujinufaisha huku wagonjwa wakiendelea kuumwa na wengine kufa,” alisema Dk Mikiwa. 
Kutokana na hilo, aliziomba serikali duniani na Wakristo wazidishe kasi ya kuombea tiba ili wanaoishikilia waitoe na wagonjwa wapewe wapone.
“Ukimwi umetuchosha, wakati vita yake bado ni mbichi kabisa, viwanda vya kutengeneza dawa fichueni siri ya tiba ya ugonjwa huu kwa sababu unatuletea umasikini, unaumiza watu na kuziingiza gharama kubwa serikali zetu.
“Yatima wanaongezeka na nguvukazi inapungua. Watu wote tumwombe Mungu ili dawa iwekwe bayana kwa sababu alikwishaileta. Tusiutumie kujipatia fedha,” alisema. 
Mbali na hilo, alizungumzia unyanyapaa kwa wenye Ukimwi na VVU na kusema bado upo na unafanywa na watu wanaoamini kuwa wao si sehemu ya jamii inayokumbwa na ugojwa huo.
Kwa maelezo yake, wanaoendekeza unyanyapaa ni wagonjwa wa akili, wagonjwa wa ujinga na waoga wa kukubali ukweli kuwa Ukimwi upo, hivyo, jamii, viongozi wa dini na serikali hawana budi kuutokomeza kwa kuelimisha wasioelewa ili watambue madhara yake kwa wanaowanyanyapaa.
Alipendekeza wanaonyanyapaa wenye Ukimwi na kuwaeleza kuwa ni watu wa kufa tu, wahukumiwe kama wauaji, lakini si kwa kunyongwa, kwa sababu haamini kama adhabu hiyo ni sahihi bali sawa na uzito wa maneno yao hayo.
Semina hiyo ya siku mbili ilihusu uandaaji vipindi vya redio na televisheni kwa wachungaji wasiopungua 30 ambao hutumia njia hizo za mawasiliano kufikisha ujumbe muhimu kwa jamii.

No comments: