Friday, November 23, 2012

WALIMU WA KIKE MIKOANI WASAKA WAUME DAR ES SALAAM...

Walimu wa kike wanadaiwa kutafuta waume Dar es Salaam, ili kupata kisingizio cha kupata uhamisho kutoka vituo vya kazi mikoani kwenda katika Jiji hilo.
Mbali na hao, wengine wamedaiwa kutumia vyeo vya waume zao kukiuka taratibu za kazi shuleni.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini alisema hayo juzi wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya maofisa elimu vifaa na takwimu wa sekondari, halmashauri na wakuu wa shule za sekondari yanayofanyika mjini hapa.
Alisema kutokana na madai mengi ya uhamisho Mkoa wa Dar es Salaam una idadi kubwa ya walimu kuliko mikoa mingine huku wakiwa na vipindi vichache zaidi darasani hadi kufikia vipindi vitatu.
Sagini alitaka walimu kuacha kutumia mbinu hizo.
“Walimu wajiandae kutumikia wananchi popote walipo na si kukaa mijini tu, shule za Dar es Salaam walimu wana vipindi vitatu tu, hivi mikoani hakuna wanaume?” Alihoji.
Alisema zamani kulikuwa na ndoa nyingi za kutengeneza, ambapo walimu  waliolewa hata na wajomba zao ili kutafuta tu kuishi mjini.
Akizungumzia matumizi ya madaraka na vyeo, alisema Kanda ya Dar es Salaam imekuwa na malalamiko mengi ya baadhi ya walimu kutumia vyeo vya waume zao kutega kazi kwa visingizio mbalimbali.
Alitoa mfano wa mwalimu wa kike ambaye alipiga simu shule aliyokuwa akifundisha ili kuomba ruhusa na alipotakiwa afuate utaratibu, alimpa simu mumewe ambaye alijitambulisha kuwa ni Kanali wa Jeshi.
“Vitu kama hivi havitakiwi, hakuna sababu ya kukiuka taratibu za kazi kwa kisingizio cha mumeo Kanali au ni nani.
Alionya kuwa Serikali haitasita kuwavua vyeo wakuu wa shule za sekondari nchini ambao wamekuwa wakinuniana na watumishi wengine, kwani ugomvi wa walimu hutokana na fedha na kutafutana uchawi.
Pia alionya wakuu wa shule nchini wanaojihusisha na migomo kuacha tabia hiyo na badala yake kama wanataka kushiriki, waachie vyeo hivyo, ili wawe na haki ya kugoma.
Sagini alisema wakuu wa shule ni miongoni mwa watu wanaoshiriki migomo ya walimu na wakati mwingine kushawishi, kitu ambacho si kizuri.
“Ukikubali cheo cha uteuzi, unatakiwa kuzingatia masharti ya uteuzi huo la sivyo unatakiwa kujivua cheo hicho, ili uwe na haki ya kugoma,” alionya.
Alisema pia ufaulu duni kitaifa hauwezi kuvumiliwa na kutaka wajipange ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
“Baadhi ya maeneo tumegundua watu hawazungumzi, itafika hatua tutawavua madaraka… wakati tunahimiza ushirikiano wengine wanatuangusha,” alisema.
Alisema jambo la muhimu ni kuheshimiana kazini na mtu usiseme ana Shahada ya Uzamili kwani umuhimu wa mtu haupimwi kwa shahada alizonazo, lazima kuwe na mkubwa kazini.
“Kwa nini walimu wengine wananyanyasa wenzao? Umepandishwa cheo si kwa maana wewe ni bora kuliko wengine, wasikilize shida zao, unakuta mwalimu darasani anakwenda kuwa Mratibu Kata kisha anajiona bora kuliko wengine!” Alishangaa.
Alitaka wakuu wa shule wanaovurunda wawekwe pembeni na washughulikiwe kama wahalifu. “Msilee tabia mbaya, lazima mchukue hatua.”  
Alisema sasa siasa zimeingia shuleni, walimu wanapiga siasa huku wana njaa. “Siasa zinaanza asubuhi umezalisha saa ngapi? Walimu pia ni wakereketwa wa siasa, wengine wana mikakati ya kutafuta majimbo, huwezi kufanya siasa ukiwa na njaa,” alisema.
Sagini pia alisema Mpango  wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) umechangia mafanikio kielimu kwani idadi ya sekondari zimeongezeka kutoka 1,745 mwaka 2005 hadi 4,528 mwaka huu.
Aidha idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne shule za Serikali na zisizo za Serikali wameongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka huu.
Kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza, alisema wameongezeka kutoka 180,239 mwaka 2005 hadi 522,379 mwaka huu huku idadi ya walimu wa sekondari ikiongezeka kutoka 18,754 mwaka 2005 hadi 65,086 mwaka huu.

No comments: