Friday, November 23, 2012

TANZANIA IKO TAYARI KUPELEKA YAKE MAJESHI KONGO DRC...

Bernard Membe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Tanzania iko tayari kupeleka kikosi cha askari wake 800 kwenda kupambana na waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), maarufu kama M23.
Amesema askari hao wa Tanzania watajiunga na askari wengine wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ili wafikie 3,200 kwa ajili ya jukumu hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Membe alisema SADC wanafikiria kupeleka Jeshi kwa kuwa alisema kuwapo kwa kikosi cha UN nchini humo hakujasaidia lolote.
“Nchi za SADC tangu mgogoro huu uanze zilishatoa azimio la kuunda jeshi litakalokwenda DRC kulinda mipaka na kupambana na M23 ili utawala uwepo Kivu, lakini UN ilisitisha nchi hizo kupeleka majeshi yake kwa madai kuwa tayari kuna vikosi vya umoja huo vya amani huko DRC,” alisema Membe.
Hata hivyo, alisema kuwapo kwa vikosi hivyo vya UN nchini humo havijasaidia lolote kutokana na kutumia kibali namba sita cha Sheria ya UN kinachotumiwa na kikosi hivyo hali iliyosababisha waasi hao waendelee kuwa na nguvu kwa kuuteka Mji wa Goma na kutishia kuuteka mji mwingine wa Bukavu.
Alisema wakati UN ikisitisha nchi za SADC na Maziwa Makuu kupeleka majeshi yake, hali nchini DRC inazidi kuwa mbaya kwa kuwa waasi hao, wanaendelea kuua na kubaka watoto na akinamama jambo ambalo linapaswa lichukuliwe hatua za haraka.
“Tunaiomba UN ikipatie kibali kikosi chake cha amani chenye askari 17,000 kilichopo DRC kikapambane na waasi hawa wa M23 au ituruhusu sisi tupeleke majeshi yetu ya askari 4,000 yanatosha kupambana na waasi hawa na kurejesha utawala DRC,” alisisitiza.
Alisema Tanzania inalaani tukio hilo la kutekwa kwa Mji wa Goma ambalo limefanyika huku mazungumzo ya amani baina ya waasi hao na Serikali ya DRC yakiendelea, lakini pia Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete walikutana kwa lengo la kutafuta suluhu la mgogoro huo.
“SADC haitokubali waasi hawa waendelee kuteka miji na ndio maana tunasikitishwa na kikosi cha UN kujiweka pembeni wakati haya yakiendelea, kesho (leo) viongozi wa nchi za SADC na Maziwa Makuu tutakutana Kampala, nchini Uganda kuzungumzia namna ya kulipatia suluhu suala hili,” alisema.
Alisema Tanzania inaisisitiza UN isikubali kushuhudia mauaji, wakimbizi wakitaabika na watu wakidhalilishwa katika nchi yao huku majeshi yao yakiangalia, ichukue hatua ama kutoa kibali kwa vikosi vyake kupambana na waasi hao au kuruhusu nchi za SADC kupeleka jeshi lake DRC.
Kikosi hicho cha M23 kilitokana na askari 1,000 waliokuwa chini ya kiongozi wa zamani wa kundi la waasi, Laurent Nkunda, ambaye askari wake takribani 4,000 walijiunga na majeshi ya Serikali ya DRC, baada  ya wasuluhishi wa mgogoro huo, marais wastaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na wa Nigeria, Olusegun Obasanjo waliposaini mkataba na waasi hao.

No comments: