Saturday, November 17, 2012

WAISLAMU WAASWA KUEPUKA MIFARAKANO...

Spika Pandu Ameir Kificho.
Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Pandu Ameir Kificho ametaka Waislamu kote nchini kuachana na mifarakano na fitna zilizopo miongoni mwao ili kuiwezesha dini hiyo kudumu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kificho alitoa rai hiyo jana Dar es Salaam wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu, zilizofanyika katika viwanja vya makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Kinondoni.
Katika sherehe hizo za kutimiza Mwaka 1434 Kiislamu, Kificho alisema ni muhimu kwa waumini wa dini hiyo kutimiza wajibu wao kikamilifu na kuachana na mambo yanayoweza kuipeleka dini hiyo pabaya, suala alilosema kuwa kwa kiasi kikubwa linaweza  kuingamiza dini.
“Kumekuwa na fikra potofu sana hasa katika kipindi hiki cha utandawazi, zinazoweza kuifanya dini itetereke na baadaye kuwa dhaifu, kama tunafika mahali tunahitilafiana na kutenda mabaya huku tukiyafumbia macho, tutakuwa tunaudhoofisha Uislamu na malipo yake Mungu pekee ndiye anajua,” alisema Kificho.
Aliongeza, kwamba ni vema Waislamu wakaunganisha nguvu pamoja na kujenga ushirikiano utakaosaidia kuipeleka dini hiyo mbele kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo kwa ilivyo kwa vizazi vilivyopo, ambapo alisema wamerithi dini hiyo kutoka kwa watu waliokuwapo zamani.
Aidha, Kificho aliwaomba  Waislamu nchini kusherehekea Mwaka huo kwa kumcha Mungu na kutenda matendo mema wakati wote kwa lengo la kutimiza waliyoaswa kufanya na Mtume Muhammad (S.A.W).
Awali, Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam Shekhe Himid Jongo, alitaka waumini wa dini hiyo kuepukana na matendo yanayoweza kuichafua huku akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake kikamilifu.
Alisema ili kutimiza wajibu huo, kila muumini anapaswa kuhakikisha anapigana na mambo machafu yanayojitokeza ndani ya dini hiyo aliyosema kuwa yanaweza kuifanya dini kudhoofika.

No comments: