Saturday, November 17, 2012

MAJAMBAZI WAJERUHI KWA MAPANGA PAROKO NA MSAIDIZI WAKE MKOANI IRINGA...

Paroko Angelo Burgeo (kushoto) na Herman Myalla wakiwa wamelazwa hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Paroko wa Parokia ya Isimani, Kanisa Katoliki wilayani hapa, Angelo Burgeo  (60) na msaidizi wake, Herman Myalla (36) wamenusurika kufa baada ya kuvamiwa na majambazi wenye silaha za moto, mapanga na nondo.
Mbali na kupigwa risasi ubavuni katika tukio hilo lililotokea saa 4.45 usiku wa kuamkia jana, Padri Burgeo alijeruhiwa kichwani kwa nondo.
Akizungumza na wanahabari katika Hospitali ya Mkoa mjini hapa ambako wamelazwa kwa matibabu, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Faustine Gwanchele alisema Padri Myalla amejeruhiwa kichwani kwa panga na nondo.
"Walifikishwa hapa saa sita usiku wa kuamkia jana, na walianza matibabu yanayoendelea mpaka sasa," alisema na kuongeza kwamba Padri Bergeo alifanyiwa upasuaji jana ili kuondoa vipande vya risasi mwilini.
Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya mlinzi wa Kanisa Katoliki Kihesa Iringa Mjini, Batholomew Nzigilwa (64) kujeruhiwa vibaya na majambazi waliovunja kanisa hilo na kuiba mali kadhaa zikiwamo zaidi ya Sh 500,000.
Dk Gwanchelle alisema hali ya Nzigilwa ni mbaya kwa sababu majambazi waliomjeruhi, walimvunja mfupa wa nyuma ya kichwa.
Awali, Ephraim Mpogole anayeishi jirani na Parokia hiyo ya Isimani aliwambia wanahabari kwamba majambazi saba walivamia makazi ya viongozi wa Parokia hiyo.
"Walivunja mlango wa kuingilia sehemu anayoishi Padri Myalla wakampiga mapanga na nondo kabla ya kumwamuru atoe fedha na kumtaka awapeleke kwa Padri Burgeo," alisema.
Akizungumza kwa shida hospitalini hapo, Padri Burgeo alisema wakati majambazi hao waliokuwa wameficha sura kwa vitambaa vyeusi wakichukua Sh milioni 1.3 kutoka kwa Padri Myalla, kwake walichukua zaidi ya Sh milioni 2.5 na simu mbili za mkononi.
Padri huyo raia wa Italia ambaye ameishi nchini kwa miaka 34 akifanya kazi ya Mungu kupitia Kanisa hilo, alisema mmoja wa majambazi hao alitaka kumwua kwa risasi baada ya jitihada zake za kutaka kukimbia kutozaa matunda.
"Walipoingia na kutaka niwape fedha na mali zingine nilizonazo nilitaka kukimbia, wakati nikifanya hivyo nilipigwa nondo kichwani na baadaye risasi na wakati nikitapatapa kwa maumivu nikawaonesha sehemu niliyokuwa nimehifadhi fedha, wakachukua na kutokomea," alisema.
Akizungumzia matukio ya viongozi wa madhehebu hayo ya dini kuvamiwa na kujeruhiwa, Bruda Augustino Kagine aliitaka Serikali na hasa Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi.
Alisema kabla ya majambazi kuvamia Parokia ya Kihesa, walivamia na kumjeruhi Paroko wa Parokia ya Nyololo wilayani Mufindi kabla ya kutokea kwa tukio hilo katika Parokia ya Isimani.
"Tumeanza kuishi kwa hofu, kwa sababu hatujui baada ya viongozi wetu hawa ni nani ndani ya Kanisa letu atafuata," alisema.

No comments: