Tuesday, November 20, 2012

TANESCO YAIKATIA RUFAA KAMPUNI YA DOWANS...

Makao Makuu ya Tanesco yaliyoko Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania, kuomba zuio la utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu iliyolitaka lilipe Sh bilioni 96 kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans.
Rufaa hiyo iliwasilishwa Septemba 19 na imepangwa kusikilizwa Desemba 5 mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji Nathalia Kimaro, Jaji Catherine Oriyo na Jaji Benard Luanda.
Tanesco wamekataka rufaa hiyo ili kusitisha utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) kama ilivyoamuliwa na Mahakama Kuu, iliyolitaka shirika hilo liilipe Dowans fedha hizo, ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba wa biashara kinyume cha sheria.
Katika rufaa hiyo, Tanesco inaomba kusitishwa kwa utekelezaji wa uamuzi huo hadi kesi ya msingi inayoendelea katika Mahakama ya Kimataifa Divisheni ya Biashara itakapokwisha.
Septemba 6, Tanesco iliwasilisha ombi hilo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam lakini Jaji Fauz Twaibu alilitupilia mbali kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Katika hukumu hiyo ya mahakama ya ICC, iliyotolewa Novemba 15 mwaka juzi, Tanesco iliamriwa kuilipa Dowans Holding SA na Dowans Tanzania Ltd (Dowans) dola za Marekani milioni 65 pamoja na riba na gharama za kuendesha kesi baada ya kuvunja mkataba na kampuni hiyo kinyume cha sheria.
Hata hivyo, Tanesco ilipinga hukumu hiyo lakini Septemba 28  mwaka jana, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu alikubali kusajili tuzo ya malipo ya Dowans na kuiamuru Tanesco kulipa fedha hizo pamoja na gharama za uendeshaji kesi.
Jaji Mushi katika hukumu yake alisema baada ya kuipitia hukumu ya ICC kabla ya kusajili tuzo hiyo, alibaini kuwa haina makosa ya kisheria kama ilivyodai Tanesco.
Kwa mujibu wa Jaji Mushi, ndani ya hukumu hiyo alikuta kiambatanisho ambacho ni mkataba kati ya Tanesco na Dowans uliosainiwa Juni 23, 2006; na kufafanua kwamba pande zote mbili katika mkataba huo zilikubaliana kwamba uamuzi wa ICC utakuwa wa mwisho, utazibana pande zote na hautakatiwa rufaa.

No comments: