Tuesday, November 20, 2012

AJALI YA MELI YA SKAGIT KUWAKALIA KOONI WATU SABA...

Baadhi ya abiria wakiwa katika harakati za kujiokoa katika ajali ya meli ya mv Skagit.
Watu saba wamependekezwa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kutokana na tuhuma za kuhusika na ajali ya meli ya mv Skagit iliyotokea visiwani hapa Julai.
Mapendekezo hayo yametolewa na Tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuchunguza ajali ya meli hiyo iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar.
Katika ripoti hiyo, imependekezwa hatua zichukuliwe kwa watu hao ili kuhakikisha kuwapo uwajibikaji kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini na watendaji wa taasisi zinazosimamia huduma hiyo na kuepusha ajali za mara kwa mara.
Akitoa taarifa jana, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Abdulhamid Yahya Mzee, alitaja watu waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwa ni pamoja na mmiliki wa meli hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa  Kampuni ya Seagull Sea Transport, Said Abdul-rahman Juma
Wengine ni nahodha wa meli hiyo, Makame Mussa Makame na Meneja wa Kampuni hiyo tawi la Dar es Salaam, Omar Hassan Mkonje.
Wahusika hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua kutokana na vitendo vyao vya kuwa karibu na sababu zilizochangia ajali hiyo, ambapo Tume inapendekeza washitakiwe kwa tuhuma za kusababisha vifo kwa uzembe.
“Mmiliki wa kampuni hiyo amefanya kosa la  kufanya biashara ya usafiri wa baharini kwa kutumia chombo ambacho hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria na hakikutimiza masharti ya ukaguzi kwa mujibu wa sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar namba 5 ya mwaka 2006.
“Ameajiri nahodha bila cheti cha umahiri cha daraja la tano na kuruhusu meli kubeba idadi kubwa ya abiria kinyume na uwezo wake,” alisema Abdulhamid.
Kwa mujibu wa taarifa,  nahodha Makame alifanya kosa la kuendesha meli bila cheti, alishindwa kuandaa abiria kujiokoa na kutoa taarifa ya dharura, pia akiendesha meli isiyo salama na kubeba abiria 431 badala ya 250 iliyoainishwa kwenye cheti cha abiria.
Wengine waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni  aliyekuwa Mkaguzi wa Meli na Kaimu Mrajisi wa Meli kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, Juma Seif Juma na Mkaguzi wa Kujitegemea Kapteni Saad Shafi Adam.
Pia inapendekezwa maofisa wa usalama wa bandari ya Dar es Salaam, Johari  Ndumbati na Peter Mwasi waadhibiwe kwa kushindwa kudhibiti uingizaji abiria kwenye meli ya mv Skagit siku iliyopata ajali ikiwa ni kinyume na majukumu yao ya kazi.
Taarifa hiyo imetoa mapendekezo ya kuimarisha Sheria na Kanuni za Usafiri wa baharini namba 5 ya 2006 kwa kuvifanyia marekebisho baadhi ya vifungu, ikiwemo kuweka utaratibu wa kisheria utakaolazimisha wafanyabiashara wa usafiri wa baharini kuwa na utaratibu wa kuuza tiketi za safari na kutengeneza urodha ya abiria kwa njia ya elektroniki.
Sheria hiyo pia inapendekezwa iweke utaratibu wa kisheria unaolazimisha uongozi wa kampuni unaoendesha biashara ya usafiri wa baharini, kuwa na taaluma ya masuala ya usafiri wa majini.
Mapendekezo mengine ni kampuni kulipa fidia abiria wote waliokuwamo ndani ya meli.  Kwa  waliopoteza maisha walipwe thamani ya kiwango cha mshahara wa chini kwa miezi 80 na walionusurika na kupata ulemavu walipwe asilimia 75 ya kiwango cha waliokufa.
Watu wengine walionusurika bila kupata majeraha walipwe asilimia 50 ya kiwango watakacholipwa marehemu.
Katika ajali hiyo watu 81 wakiwamo raia watatu wa kigeni waliokufa maji na miili yao kupatikana na kuzikwa. Watu wengine 212 walipotea na 154 waliokolewa wakiwa hai wakiwamo raia 15 wa kigeni.
Katibu Mkuu Kiongozi alisema Tume imeeleza sababu za kutokea ajali hiyo, kuwa ni upepo mkali, muundo wa meli ikuruhusu abiria wengi kukaa juu, mwendo kasi, nahodha kukosa ujuzi na umahiri, pamoja na abiria kuwa wengi kupita kiasi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekubaliana na mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe 10 chini ya uenyekiti wa  Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Abdulhakim Ameir Issa.

No comments: